1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Klitschko: Ninaendelea kuyanoa makali

19 Oktoba 2015

Wladimir Klitschko atayaweka ulingoni mataji yake ya ulimwengu ya WBA, WBO na IBF wakati atakapoangushana na bondia Muingereza Tyson Fury mjini Düsseldorf, Ujerumani mnamo November 28

https://p.dw.com/p/1GqYC
Hayden Panettiere und Wladimir Klitschko
Picha: Getty Images

Pigano hilo lilikuwa limepangwa awali kufanyika Oktoba 24, lakini likaarishwa baada ya Klitschko kukumbwa na maumivu ya nyonga katika kambi yake ya mazoezi.

Mukraine huyo mwenye umri wa miaka 39 ameahidi kuwa hatompuuza Fury "Bila shaka, mimi huwa na woga kabla ya kila pigano. Ni changamoto. Hauwezi kusema, kuwa nitafaulu, kwamba nitaenda kushinda pigano hili. Bila shaka hilo ndio lengo langu na hilo ndio ninalowazia hakuna fikira nyingine zozote. Lakini inategemea na kazi nyingi, kuwa makini na nidhamu na ninasubiri sana pigano lijalo. Tyson Fury hakika ni mrefu kuniliko na ngumi nzito kuniliko. Ana malengo yake, na nimekuwa nikishamiri katika mchezo huu kwa muda mrefu lakini ni vigumu sana kuyatetea mataji yako baada ya miaka mingi, ming, mingi sana".

Klitschko atapigana na Fury akiwa na rekodi ya ushindi mara 64 ambapo 53 ni kwa njia ya knock out na amechapwa mara tatu. Lakini hajashindwa katika mapigano yake 22 ya mwisho tangu Oktoba 2004 wakati alipoangushwa sakafuni na Mmarekani Lamon Brewster.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu