Klopp: Borussia Dortmund itajipanga upya
22 Desemba 2014Jibu ni kuwa Mjerumani huyo haendi kokote, angalau kwa sasa….hii ni baada ya Mkurugenzi wa Spoti wa klabu ya Dortmund Michael Zorc kuthibitisha kuwa Klopp ataendelea kuifunza timu hiyo inayoyumba.
Zorc amesema amefanya mkutano wa saa kadhaa na Klopp na Mkurugenzi Mkuu Hans-Joachim Watzke ambapo walikubaliana kuwa watashirikiana na wanaamini watafanya kila liwezalo ili kujiondoa katika hali hiyo mbaya.
Klopp ambaye amekuwa na klabu hiyo tangu mwaka wa 2007, amesisitiza hata baada ya siku ya Jumamosi kupokea kichapo cha kumi katika mechi 17, kuwa haendi kokote. Alisema ni wakati mgumu kwa kila mtu anayeipenda klabu hiyo lakini anaamini itafufuka tena akiongeza kuwa wanayo fursa ya kuimarika na anaamini hivyo ndivyo itakavyokuwa katika mzunguko wa pili wa msimu.
Lakini wakati Klopp akielezea matumaini ya mambo kuimarika baada ya kipindi cha mapumziko ya msimu wa baridi, nahodha wake Mats Hummels anasema hakuna uhakika kuwa Borussia Dortmund itakwepa kushushwa daraja ifikapo mwezi Mei.
Hummels anasema karibu kila wachezaji wao nyota wa kikosi cha kwanza walikosekana wakati mmoja katika nusu ya kwanza ya msimu na hawakuwa imara kwa asilimia 100.
Anasema wanastahili kufanikiwa kuwa na kila mchezaji mzima wakati wa kipindi hiki cha mapumziko, kisha wataweza kuonyesha timu mpya wakati wakiwa na wachezaji bora kama 15 au 16 hivi.
Dortmund tayari wamefuzu kama washindi wa kundi mbele ya Arsenal katika hatua ya 16 bora ya ligi ya mabingwa wa Ulaya - Champions League, ambapo wamepangwa na Juventus, lakini wamekuwa na mwanzo mbaya zaidi katika msimu wa Bundesliga kuwahi kuhushudiwa katika miaka 27.
Mwandishi. Bruce Amani/AFP
Mhariri. Gakuba Daniel