1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kocha Klose ajiunga na Bayern Munich

Josephat Charo
9 Mei 2020

Miroslav Klose "The Quiet One" anayeshikilia rekodi ya kufunga mabao mengi katika mashindano ya kombe la dunia la kandanda kwa wanaume, amejiunga na Bayern Munich kama kocha msaidizi.

https://p.dw.com/p/3bysE
Deutschland Klose
Picha: Imago Images/Sven Simon/F. Hoermann

"Ni hisia nzuri sana, nasubiri kwa hamu kubwa kuanza kazi," alisema mchezaji huyo wa zamani timu ya taifa ya kandanda ya Ujerumani mwenye umri wa miaka 41, liyefunga magoli 16 katika mashindano manne ya kombe la dunia na kushinda kombe na timu ya taifa Die Mannschaft 2014 nchini Brazil.

Klose atakuwa katika kikosi cha kiufundi cha Bayern ligi kuu ya kandanda ya Ujerumani, Bundesliga, itakapoanza tena Mei 16 tangu ilipositishwa katikati ya mwezi Machi kutokana na janga la virusi vya corona, huku Bayern ikiwa na miadi na Union Berlin Jumapili Mei 17.

Mchezaji huyo wa zamani wa Bayern Munich anasema kujiunga na klabu yake ya zamani ni hatua nyingine mbele katika kazi yake ya ukufunzi baada ya kufanya kazi na timu ya vijana wa umri wa chini ya miaka 17 kwa misimu miwili iliyopita.

Klose alisaini mkataba hadi Juni 2021 unaomuunganisha na kocha wa Bayern, Hansi Flick, kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Ujerumani wakati wa mashindano ya kombe la dunia 2014. "Tunaamiana kitaaluma na kibinafsi," alisema Klose kumhusu Flick.

Rekodi ya Klose uwanjani ni bayana kabisa akiwa na jumla ya mabao 71 katika mechi 137 alizoichezea timu ya taifa ya Ujerumani.

"Kutokana na uzoefu wake kama mchezaji wa soka la kulipwa katika ngazi ya juu kabisa ya kimataifa, 'Miro' ni chaguo mujarab na kamili kwa kikosi chetu cha makocha," alisema Flick.

Klose pia alifunga magoli 53 katika mechi 150 alizoichezea Bayern, kabla kuondoka na kuhamia Lazio mwaka 2011 na kustaafu baada ya miaka mitano nchini Italia.

"Ndiye mshambuliaji wa Ujerumani aliyefanikiwa zaidi katika miaka 15 hadi 20 iliyopita," alisema mwenyekiti wa klabu ya Bayern, Karl-Heinz Rummenigge, aliyemueleza Klose kama 'kocha mwenye ndoto'.

"Washambuliaji wetu hasa watanufaika sana kutoka kwake kama kocha".

(afp)