1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Koehler ajiuzulu kama mjumbe wa Sahara Magharibi

23 Mei 2019

Umoja wa Mataifa umesema siku ya Jumatano (23.05.2019) kwamba mjumbe wake maalumu kwa ajili ya Sahara Magharibi, Horst Koehler, amejiuzulu wadhifa wake kutokana na sababu za kiafya.

https://p.dw.com/p/3IvtB
Schweiz Vereinte Nationen- Westsahara | Horst Köhler
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Trezzini

Koehler, rais wa zamani wa Ujerumani, aliteuliwa Agosti 2017 kuongoza juhudi za Umoja wa Mataifa kuumaliza mzozo wa miongo kadhaa kati ya Morocco na chama cha Polisario kinachoungwa mkono na Algeria.  Mjumbe huyo mwenye umri wa miaka 76 aliwasilisha taarifa hiyo kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, katika mazungumzo ya simu siku ya Jumatano, taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema.

Guterres amesikitishwa sana na kujuzulu huko kwa Koehler lakini akasema anaelewa kikamilifu uamuzi huo na kumtakia kila la kheri, ikaongeza taarifa hiyo. Amemshukuru Koehler kwa juhudi zake thabiti na kubwa ambazo ziliweka msingi wa kasi mpya katika mchakato wa kisiasa kuhusiana na suala la Sahara Magharibi.

Katika taarifa, wizara ya mashauri ya nchi za kigeni ya Morocco ilisema ufalme wa Morocco unatambua kwa masikitiko kujiuzulu kwa Koehler, huku ukimpongeza kwa juhudi zake alizozifanya tangu alipoteuliwa.

Chama cha Polisario kwa upande wake kimesema kimehuzunishwa sana na taarifa hizo na kumshukuru mjumbe huyo anayeondoka kwa jitihada zake kubwa kuufufua mchakato wa amani wa Umoja wa Mataifa. Kuondoka kwa Koehler kunayaacha mazungumzo ya upatanisho ya Umoja wa Mataifa katika mkwamo kufuatia duru mbili za mazungumzo zilizoashiria kurejea kwa mara ya kwanza pande zinazohasimiana katika meza ya mazungumzo katika kipindi cha miaka sita.

Chama cha Polisario kilipigana vita na Morocco kuanzia 1975 hadi 1991 wakati mkataba wa kusitisha mapigano ulipoafikiwa na tume ya amani ya Umoja wa Mataifa ikapelekwa kusimamia utekelezaji wa mkataba huo. Chama hicho kinataka kura ya maoni kuhusu uhuru, kitu ambacho Morocco imekataa katakata. Morocco, ambayo ililiteka eneo hilo baada ya Uhispania kuondoka mnamo mwaka 1975, inaichukulia Sahara Magharibi kama sehemu ya ufalme wake na badala yake imelipa eneo hilo utawala wa ndani.

Koehler alihudumu kama rais wa Ujerumani kuanzia 2004 hadi 2010 na alikuwa mkurugenzi mkuu wa shirika la fedha la kimataifa IMF kuanzia 2000 hadi 2004.

(afpe, dpae)