1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Koffi Annan awaomba wadhamini kutoa misaada zaidi ili kudhibiti hali ilivyo Darfur.

Josephat Charo22 Julai 2004

Umoja wa Mataifa unakabiliwa na upungufu wa fedha za kuwasaidia watu zaidi ya milioni mbili waliowachwa bila makao kwa sababu ya vita katika eneo la Darfur huko Sudan. Katibu mkuu wa umoja huo bwana Koffi Annan amewaomba wadhamini wa kimataifa kujitolea kifedha haraka iwezekanavyo ili kudhibiti hali hiyo.

https://p.dw.com/p/CEHs
Sudan Darfur
Sudan DarfurPicha: AP

Akizungumza na waandishi wa habari Annan alisema pesa na nishati zaidi zinahitajika kwa dharura ili kuweza kutoa huduma za binadamu kwa watu hao wa Darfur walio katika shida kubwa. Umoja wa Mataifa unahitaji dola milioni 349 kwa ajili ya wakimbizi huko Darfur na Chad lakini kwa sasa umoja huo umeahidiwa kupewa dola milioni 145 pekee kutoka kwa wahisani. Bwana alielezea wasiwasi wake kwamba ikiwa pesa hizi zitachelewa kupatikana, huenda watu wengi wakapoteza maisha yao kwa ukosefu wa chakula na huduma muhimu.

Annan aliongeza kusema kwamba bado kuna dola milioni 204 zinazohitajika kuafanya kazi hiyo. Aliwahimiza wadhamini kutimiza ahadi zao walizotoa na pia kuongeza viwango vya miaada yao. Annan alisisitiza kuwa msaada unaohitajika ni wa vifaa hasa ndege sita aina ya helikopta zitakazotumiwa kupeleka chakula na mahitaji mengine katika maeneo ya Darfur hasa ikizingatiwa kwamba mvua tayari imeanza kunyehs kwa wingi na barabara hazipitiki.

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa na Marekani zimeishurutisha serikali ya Sudan kukomesha matendo maovu yanayotekelezwa na kundi la Janjaweed na wanamgambo wengine wa kiarabu. Wanamgambo hawa wamekuwa wakiua, kubaka na kuwakata watu mikono katika kampeni yao ya kikabila ya safisha safisha. Pia wameendelea kuchoma moto vijiji vya waafrika katika eneo la Darfur. Ikiwa serikali hiyo imeshindwa kukabiliana na wanamgambo hao, basi inatakiwa kwa haraka kutafuta msaada kutoka kwa jamii ya kimataifa.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani bwana Collin Powel na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Koffi Annan watakutana leo huko Sudan ili kujadili hali ilivyo sasa. Viongozi hawa wanafanya kila wawezalo kukabiliana na hali ya Darfur ambayo imeelezwa na mashika ya misaada ya kiutu kuwa mauaji ya halaiki na ya kikabila. Maafisa wa Marekani wanawahoji wakimbizi ili kujua ikiwa hali hiyo kweli imefikia kiwango cha kuitwa mauaji ya halaiki jambo ambalo litasababisha hatua zaidi kuchukuliwa na jamii ya kimataifa.

Annan amesema Sudan haijajitolea kwa dhati kukabiliana na wanamgambo wa kiislamu nchini humo na akaonya kwamba huenda jamii ya kimataifa ikalazimika kuingilia kati ili kukomesha mauaji na ghasia zao. Msemaji wa idara ya ulinzi ya Marekani bwana Richard Boucher amesema huko mjini Washington kwamba hali ya Darfur ni jambo ambalo limewatatiza wanachama wote wa baraza la usalama. Aidha alisema wakati umewadia wa baraza hilo kujadili tatizo la Darfur na kuchukua hatua zinazofaa.

Kadri watu elfu 30 wameuwawa katika vita vya Darfur ambavyo vimekuwa vikiendelea kwa miezi 15. Watu kadri milioni 2.2 wamewachwa bila makao huku mamia ya maelfu wakiwa wamevuka mpaka na kukimbilia nchi jirani ya Chad. Annan na Powell wanatarajiwa kujadili hatua za baraza la usalama la umoja wa mataifa ambazo huenda zichukuliwe ikiwa Sudan haitatimiza ahadi zake ilizotoa wakati viongozi hawa walipozuru Sudan katika safari yao ya awali.

Habari zaidi zinasema kwamba ripoti mpya iliyotolewa na kundi la wachambuzi walio na uhusiano na kundi la Sudan Peoples Liberation Army,SPLA, inaeleza kuwa katika eneo la kusini mwa Sudan ambako huduma za serikali hazipo, wasichana wanakabiliwa na hatari kubwa ya kufa wakiwa wajawazito ama wakati wanapojifungua ikilinganishwa na uwezo wao wa kumaliza masomo ya shule ya msingi. Watoto elfu 95 wa umri chini ya miaka mitano walifariki kwa sababu ya maganjwa katika mwaka wa 2003.