Kombora la Urusi lawauwa watu 16 madukani Ukraine
28 Juni 2022Kombora la Urusi lililolipiga jengo kubwa la maduka ambalo lilikuwa limefurika watu katikati mwa Ukraine limewauwa watu 16. Viongozi wa kundi la nchi saba tajiri duniani - G7 wanaoukutana nchini Ujerumani wamesema tukio hilo ni uhalifu wa kivita.
Soma pia: Viongozi wa G7 waapa kuisaida Ukraine "bila kuchoka"
Wameapa kuwa Rais wa Urusi Vladmir Putin na wote waliohusika watawajibishwa kwa shambulizi hilo la mji wa Kremenchuk. Ukraine imeituhumu Urusi kwa kuwalenga raia makusudi. Rais Volodymyr Zelensky ameliita shambulizi hilo kuwa ni moja ya vitendo vikubwa kabisa vya kigaidi kuwahi kufanywa katika historia ya Ulaya.
Soma pia: Viongozi wa G7 kuilenga sekta ya mafuta ya Urusi
Katika mashambulizi mengine tofauti, makombora ya Urusi yaliwauwa karibu raia wanane wakati wakichota maji katika mji wa mashariki wa Lysychansk. Na shambulizi mjini Kharkiv liliwauwa watu wanne na kuwajeruhi wengine 19.
Ukomo kwa bei za mafuta ya Urusi
Viongozi katika mkutano wa kilele wa - G7 unaoingia siku yake ya tatu na ya mwisho leo wamepiga hatua kuhusu kuweka ukomo wa bei kwenye bidhaa za mafuta kutoka Urusi.
Soma pia: Hali ngumu Lysychansk Ukraine
Hatua hiyo inajiri wakati viongozi wa ulimwengu wakitafuta mbinu za kuzuia mapato ya nishati ya Moscow. Mipango mipya ya vikwazo vilivyoimarishwa ambavyo vinaathiri sekta ya mafuta na jeshi la Urusi ilitangazwa wakati Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akiuhutubia mkutano huo jana kwa njia ya video.
Alitoa ombi kwa kundi la G7 kutoa msaada wa mifumo ya ulinzi wa mashambulizi ya angani, uhakikisho wa usalama, kusaidia katika uuzaji wa nafaka iliyokwama kwenye bandari za Ukraine, vikwazo zaidi dhidi ya Urusi na msaada wa kuijenga upya Ukraine. Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani ndiye mwenyeji wa mkutano wa kilele wa G7 mwaka huu katika Milima ya Bavaria, na viongozi wa Uingereza, Canada, Ufaransa, Italia, Japan na Marekani. Viongozi wa Afrika Kusini, Senegal, Argentina, India, na Indonesia pia wanahudhuria.
afp