Kongamano la kuichangia fedha Sudan lafanyika Ufaransa
15 Aprili 2024Juhudi hizo ni kupitia kongamano la wafadhili linalofanyika leo mjini Paris Ufaransa, ambapo ni mwaka mmoja tangu mzozo wa Sudan kuzuka Aprili 15, baada ya mvutano wa muda mrefu kuzuka na kusababisha mapigano makali kati ya jeshi na kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF)
Shirika la habari la Reuters limesema Marekani inapanga kutangaza fedha zaidi ya dola milioni 100 za msaada katika kongamano hilo linalotarajiwa kuhudhuriwa na Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Stéphane Séjourné, mwenzake wa Ujerumani Annalena Baerbock, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borell na Kamishna wa Umoja huo wa shughuli za usimamizi wa migogoro Janez Lenarcic.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan vimeharibu vibaya miundombinu, kuiweka nchi hiyo katika hatari ya kukabiliwa na baa la njaa na kusababisha raia wengi kupoteza makaazi yao.