1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongamano la Uchumi duniani lafunguliwa, Davos

23 Januari 2018

Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi atafungua kongamano la uchumi duniani, WEF linalofanyika mjini Davos, Uswisi. Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kuhutubia kongamano hilo siku ya Ijumaa.

https://p.dw.com/p/2rLkY
Schweiz WEF 2018
Picha: World Economic Forum/M. Nutt

Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi hii leo anafungua kongamano la mwaka huu la uchumi duniani, WEF linalofanyika mjini Davos, Uswisi. Masuala ya kisiasa yatachukua nafasi muhimu kwa kuwa linahudhuriwa pia na wanasiasa wengi ikiwa ni pamoja na Rais wa Marekani Donald Trump.

Waziri mkuu wa Canada Justin Tradeau anatarajiwa kuwasilisha ajenda kuu ya mwaka huu ya mataifa yaliyoinukia kiuchumi G7. Canada inachukua uenyekiti wa kundi hilo mwaka huu.

Ajenda kuu ya mwaka huu ya kongamano hilo la WEF ni "mustakabali wa pamoja katika dunia iliyofarakana". Ajenda hii inapingana moja kwa moja na sera ya rais wa Marekani Donald Trump ya "Marekani kwanza" inayohusisha sheria za kulinda soko la Marekani na sera za kujitenga. 

Donald Trump
Rais wa Marekani Donald Trump atahutubia kongamano hilo linalosisitiza utangamano katika kukabiliana na changamoto za kidunia.Picha: AP

Mwanzilishi wa Kongamano hilo la  Kiuchumi Duniani Klaus Schwab amesema kuna hatari iliyo dhahiri katika nyakati hizi ya kuvurugika kwa mfumo wa kidunia. Amesema hakuna namna yoyote ya kukabiliana na hali hiyo iwapo hakutakuwa na ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia, suala ambalo jukwaa hilo linalisimamia.

Rais wa kongamano hilo Borge Brende aliwaambia waandishi wa habari, akisema kusanyiko la wakuu 70 wa serikali mbalimbali duniani pamoja na wafanyabiashara wenye nguvu duniani kunaweza kuleta mchango muhimu kuelekea kukabiliana na vikwazo vya sasa katika sekta ya biashara duniani.

Donald Trump anayesifika kwa sera za kujitenga atahutubia kongamano hilo, Ijumaa.

Rais wa Marekani, Donald Trump anatarajiwa kuhutubia kongamano hilo siku ya Ijumaa, ambayo ni siku ya mwisho ya kongamano hilo.Tangu alipochukua madaraka mwaka mmoja uliopita, Trump amechangia kwa kiasi kidogo katika kuunga mkono masuala ya utandawazi na utangamano, ambayo yanapewa nafasi kubwa katika kusanyiko hilo la Davos.

Frankreich Emmanuel Macron empfängt Bundeskanzlerin Angela Merkel in Paris
Kansela Angela Merkel akiwa na rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: picture-alliance/dpa/MAXPPP/T. Padilla

Siku mbili kabla ya rais huyo kuhutubia, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anatarajiwa pia kutoa hotuba yake itakayohusu kimashirikiano ndani ya Umoja wa Ulaya. Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Seibert amesema Ujerumani ni mshirika muhimu katika masuala ya kiuchumi na siasa ndani ya Umoja huo wa Ulaya na inajihusisha kwa sehemu kubwa katika mijadala ya kisiasa kuhusu mustakabali wa kimaendeleo wa Umoja huo, na ndio maana kansela Merkel amechagua kueleza mawazo yake kuhusu Umoja wa Ulaya kwenye kongamano hilo la Davos.

Merkel atazungumza siku moja pamoja na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron.

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, Papa Francis kwa upande wake amewataka wafanyabiashara na wanasiasa katika kongamano hilo kuandaa mazingira yatakayoruhusu ujenzi wa jamii inayohusisha makundi yote. Alituma ujumbe huo kwa washiriki wa kongamano hilo la Davos, baada ya ziara yake nchini Chile na Peru. 

Papa Francis amesema wafanyabiashara wana nafasi muhimu ya kuleta mabadiliko, ambayo ni pamoja na  kuuunda nafasi za ajira mpya, kuheshimu sheria za kazi , kukabiliana na ufisadi na pia kuhamasisha haki ya jamii.

Kongamano hilo linalomazika siku ya Ijumaa, linawakutanisha zaidi ya washiriki 3,000 ambao miongoni mwao ni wanasiasa, wasomi, wakuu wa serikali, pamoja na viongozi wa taasisi za fedha dunia na makundi muhimu yasiyo ya kibiashara.

Mwandishi: Lilian Mtono/http://www.dw.com/en/world-economic-forum-in-davos-out-to-heal-a-fractured-world/a-42228090/APE/EAP.

Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman