Kongamano la uchumi juu ya Afrika lamalizika
5 Mei 2017Chama cha Africa National Congress ANC, kilitumbukia kwenye migogoro zaidi pale rais Jacob Zuma alipomtimua aliyekuwa waziri wa fedha Pravin Gordhan mnamo mwezi wa tatu alipofanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri ambapo maswahiba wa rais Zuma walitunukiwa madaraka.
Mamia ya wawakilishi wa biashara, wanasiasa na watalaamu wanahudhuria kongamano hilo linalomalizika leo hii katika mji wa pwani wa Durban nchini Afrika Kusini.
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolgang Schaeuble ameieleza DW juu ya mpango wa nchi 20 zilizostawi kiuchumi G20 wa kuleta maendeleo endelevu katika bara la Afrika. Schaeuble amesema mpango huo sio kwa ajili ya misaada tu bali ni wa kuweka mazingira endelevu barani humo ili bara la Afrika liweze kushiriki ipaswavyo kwenye uchumi katika siku za usoni
Wakati kongamano hilo likiendelea hapo jana jaji wa mahakama kuu ya nchini Afrika Kusini alitoa maamuzi yaliyomuagiza rais Jacob Zuma aeleze uhalali wa hatua yake ya kulipangua baraza lake la mawaziri.
Rais Zuma alitetea hatua yake hiyo kwa kusema kuwa ni kweli alilibadili baraza lake la mawaziri lakini amelibadilisha kwa kuwaweka vijana ijapokuwa anatambua kuwa watu wengine watakuwa na maoni tofauti. Waziri aliyechukua mahala pa waziri wa fedha wa zamani Pravin Gordhan ambaye ni Malusi Gigaba alikuwepo katika kongamano hilo ambapo Afrika Kusini ndio mwenyeji.
Waziri huyo mpya aliwaambia waandishi wa habari kwamba amechoka kujibu maswalai yanayohusu iwapo Zuma atashindwa bungeni baada ya kura ya kutokuwa na imani naye kupigwa. Gigaba amesema hakuna nafasi kamwe ya Zuma kushindwa na kwamba kura kama hiyo haina nafasi katika bunge la Afrika Kusini.
Chama cha ANC kina asilimia 62 katika bunge la nchi hiyo. Kumekuwepo kura nyingi za kutokuwa na imani na rais Zuma lakini hazikufaulu. Wawakilishi wa biashara za kimatafa hata hivyo wameelezea wasiwasi wao kutokana na mabadiliko aliyoyafanya rais Zuma katika baraza lake.
Ni katika kongamano hilo ndipo rais Jacob Zuma alipozungumza kwa mara ya kwanza kuhusu kuzomewa katika siku ya wafanyakazi duniani iliyoadhimishwa hapo Mei mosi na kukilaumu chama cha wafanyakazi nchini Afrika Kusini COSATU ambacho kina mahusiano ya kisiasa na chama cha ANC kwa kuandaa fujo dhidi yake. Zuma amesema watu bado hawaelewi maana halisi ya demokrasia ijapokuwa kuzomea na kuzusha mijadala vyote hivi ni miongoni mwa demokrasia lakini kwa bahati mbaya watu hawaelewi vyema wanautumia vibaya uhuru huo.
Rais Zuma alizomewa na kundi kubwa la watu linaloaminiwa kuwa ni wafanyakazi katika mji wa Bloemfontein ambapo walinzi wa rais Zuma walilazimika kumuondoa rais huyo na hivyo kusababisha kuvunjwa shughuli iliyokuwa imepangwa.
Rais Zuma analaumiwa kwa kutumia mabavu na kushiriki vitendo vya rushwa katika utawala wake.
Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE
Mhariri: Iddi Ssessanga