Vijana wa Afrika na Ulaya wajadili uwajibikaji na Umoja
7 Mei 2019Akizungumza katika kongamano la siku tatu linalofanyika mjini Bonn nchini Ujerumani, mjumbe maalumu wa Umoja wa Afrika anayehusika na masuala ya vijana Aya Chebbi amesema, pamoja na changamoto ambazo umoja wa Afrika unakumbana nazo katika kuwapa vijana jukwaa la kubadilishana uzoefu, lengo kubwa la umoja huo ni kusaidia kuwafikia vijana popote walipo hasa walio vijijini, pembezoni na ambao hawapati taarifa kutokana na kukosa huduma za mtandao wa mawasiliano wa intaneti.
"Nadhani kwa kizazi chetu ni muhimu zaidi kuvuka mipaka na tofauti mbalimbali. Ni muhimu kwa kuwa kizazi chetu ni cha ulimwengu ambao wanaamini katika dunia isiyo na mipaka.''
Mtandao wa Intaneti kikwazo katika kusambaza taarifa
Chebbi amesema vijana wanatafuta uhuru na kujieleza kama na ndio maana hivi sasa wamehamia kwenye jukwaa la mtandao kwa sababu ni mahali wanaweza kupata nafasi ya kujadili kwa uwazi.
Mwakilishi huyo wa vijana wa umoja wa Afrika ameongeza kuwa, pamoja na vijana kufunguliwa dirisha la dunia kupitia mtandao, bado vijana wengi wa kiafrika hawapati mtandao kwani asilimia 70 ya watu barani Afrika hawana huduma hiyo, jambo linalofanya upatikanaji na usambazaji wa taarifa kutokuwa na usawa duniani.
Mshiriki wa kongamano hilo kutoka Tanzania Lidya Richard Maika amesema kupitia kongamano hilo amejifunza mengi ikiwemo namna nchi yake inavyoweza kushirikianana nchi za nyingine za Afrika kufanya programu za mabadilishano ya vijana kupitia taasisi anayoifanyia kazi.
Kongamano hilo la vijana linakamilika siku ya Jumatano, na nchi za Benin, Tanzania, Afrika ya kusini zinashiriki kama nchi za majaribio za programu ya kubadilishana uzoefu ambayo itakamilika mwaka 2020 na kuandaliwa na Taasisi ya Engagement Global kwa kushirikiana na France Volontaires, Taasisi ya ushirikiano ya Norway NOREC chini ya ufadhili wa wizara ya maendeleo na ushirikiano wa kiuchumi ya Ujerumani.