1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo na SADC kuanzisha operesheni ya pamoja

Saleh Mwanamilongo
16 Januari 2024

Jeshi la Kongo limetangaza kuanzisha operesheni ya pamoja na wanajeshi wa kikosi cha Jumuiya ya nchi za SADC dhidi ya waasi wa M23 Mashariki mwa Kongo.

https://p.dw.com/p/4bKlg
Wanajeshi wa Afrika Kusini tayari wamewasili Goma
Wanajeshi wa Afrika Kusini tayari wamewasili GomaPicha: RAJESH JANTILAL/AFP

Viongozi wa kijeshi wa Kongo na wale wa kikosi cha mataifa ya Jumuiya ya mataifa ya kusini mwa Afrika SADC, wamefanya mkutano wa tahmini ya hali ya kiusalama jimboni Kivu ya Kaskazini. Kufuatia mkutano huo, Luteni Jenerali Fall Sikabwe, kaimu mkuu wa jeshi la Kongo amesema jeshi la FARDC na kikosi cha SADC maafuru SAMIDRC wataanzisha operesheni ya pamoja dhidi ya waasi wa M23.

'' Raia wafahamu kwamba SADC imekuja kwa mapambano'', alisema Sikwabwe.

Kwa upande wake, naibu kamanda wa kikosi cha SADC nchini Kongo , Jenerali Julius Gambos kutoka Tanzania amesema lengo la kikosi hicho ni kuunga mkono jeshi la Kongo kuyasaka makundi ya waasi huko kwenye majimbo ya mashariki.

''Kama kutakuwa na wapiganaji ambao wanaipinga serikali basi tutaungana na majeshi ya serikali ya Kongo kuhakikisha kwamba tunawatoa.'', Gambos aliwaambia waandishi habari mjini Goma.

Kikosi hicho cha SAMIDRC kinajumuisha wanajeshi kutoka Malawi, Afrika Kusini, na Tanzania. Kundi la kwanza la wanajeshi wa kikosi hicho kutoka Afrika Kusini liliwasili mjini Goma Desemba 15.

''EAC ilianza vibaya''

Wanajeshi wa Kenya wa Kikosi cha EAC
Wanajeshi wa Kenya wa Kikosi cha EACPicha: Alexis Huguet/AFP

Serikali ya Kongo ilialika kikosi hicho cha SADC baada ya kusema kuwa haijaridhika na wanajeshi wa jumuiya ya Afrika Mashariki EAC ambao walitakiwa kupambana na waasi wa M23. Kikosi cha EAC likiondoka Desemba baada ya mwaka mmoja huko Kivu ya Kasazini. Steward Muhindo, mtafiti na mwanaharakati wa kundi la kutetea Demokrasia nchini Kongo , Lucha, aliiambia DW kwamba wanategemea kuwa kikosi hiko cha SADC kitafanikiwa katika kazi yake, kinyume na kile cha EAC.

"Nitakacho sema ni kwamba , tofauti na kikosi cha SADC, kile cha EAC kiliundwa na nchi ambazo kwa namna moja au nyingine zilichangia kuyumbisha usalama wa Kongo, kwa hiyo kwa mtazamo huu, EAC ilianza vibaya na pili muhula wake haukujulikana ikiwa walitakiwa kupigana na waasi wa M23 au kulinda amani na kujihami,'' alisema Steward Muhindo.

Kikosi cha jumuiya ya SADC, SAMIDRC kitaongozwa na Meja- Jenerali Monwabisi Dykopu kutoka Afrika Kusini na kaimu wake ni kutoka Tanzania. Jenerali Monwabisi analifahamu vyma eneo hilo la mashariki mwa Kongo, kwa sababu alikuwa moja ya makamanda wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, Monusco. Huku hayo yakijiri kuliripotiwa mapigano makali hapo jana baina ya jeshi na waasi wa M23 huko mtaani Masisi, jimboni Kivu ya Kaskazini.