1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo yawasilisha shauri jipya katika mahakama ya ICC

24 Mei 2023

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa mara nyingine imepeleka rasmi shauri katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC.

https://p.dw.com/p/4RkOJ
Demokratische Republik Kongo | Soldaten der EACRF und M23 Rebellen in Kibumba
Picha: GLODY MURHABAZI/AFP/Getty Images

Kuhakikisha mahakama hiyo inashughulikia  kile inachokiita uporaji wa kupangwa wa rasilimali zake mashariki mwa nchi hiyo, unaofanywa na jeshi la Ulinzi la Rwanda na kundi la waasi la M23. 

 ICC tayari ina uchunguzi unaoendelea mashariki mwa Kongo tangu mwaka 2004 na haijabainika iwapo shauri jipya lililowasilishwa na Kongo litaubadilisha mwelekeo wa mahakama hiyo.

Soma pia: Wanamgambo watikisa usalama Kinshasa

Katika taarifa yake Wizara ya sheria ya Kongo imesema serikali  ina wasiwasi mkubwa juu ya mateso ya wananchi wake  katika sehemu ya eneo lilioathiriwa na vitendo vilivyotajwa katika kesi hii.

Soma pia: Zaidi ya raia 130 wauawa na waasi wa M23 yasema ripoti ya UN

Aidha wizara hiyo imesema kwamba lengo la kupeleka shauri hilo katika mahakama ya ICC ni kutaka uchunguzi ufanyike  na kufunguliwa mashtaka dhidi ya yeyote aliyehusika katika ukiukaji wa haki za binadamu kati ya 2022 na 2023.

Maelezo ya shauri la Kongo

Kundi la waasi la M23 linaloongozwa na Watutsi lilianzisha mashambulizi mapya mashariki mwa Kongo mwezi Machi mwaka jana, na kuteka miji na vijiji katika eneo linalopakana na Uganda huku mapigano hayo yakilazimisha zaidi ya watu milioni 1 kukimbia makaazi yao.

Uganda | Binnenvertriebene aus dem Rutshuru-Territorium
Picha: BADRU KATUMBA/AFP/Getty Images

Kongo imeishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono M23, ingawa serikali ya Rwanda imekanusha kuhusika kwa namna yoyote ile.

Ofisi ya mwendesha mashtaka wa ICC haijatoa maelezo mengine zaidi ya kwamba lengo ni kufuatilia madai ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu uliofanywa kuanzia Julai 2002 katika eneo la Ituri na Mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini.

Mwendesha Mashtaka mkuu  wa ICC Karim Khan anatarajiwa kuitembelea Kinshasa na majimbo mengine ya Kongo yaliyoathiriwa na makundi ya waasi kuanzia Mei 28 hadi Mei 31.

Kufikia sasa ICC imewatia hatiani Wakongo watatu ambao ni viongozi wa wanamgambo, mmoja kwa uhalifu wa kivita, wengine kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu kwa kuhusika katika ukatili uliofanywa mashariki mwa Kongo.

Soma pia: Ntaganda : Mahakama ya ICC yaunga mkono hukumu ya mwanzo

Haya yanajiri huku rais wa Jamuhuri ya kidemkorasia ya Kongo Felix Tshisekedi, akitarajiwa kufanya ziara nchini China kuanzia leo tarehe 24 Mei hadi tarehe 29.