Korea Kaskazini bado inataka mwafaka na Marekani
1 Machi 2019Kauli kali ambazo zilifuatia mazungumzo ya mwanzo yaliyoshindwa kuhusiana na mpango wa silaha za kinyuklia wa Korea kaskazini na vikwazo, hazikuwapo kwa kiasi kikubwa mara hii, lakini kulikuwa na hali ya kuutangaza mkutano huo wa siku mbili katika mji mkuu wa Vietnam, Hanoi kwa kiasi fulani kwa hali ya tahadhari.
Kichwa cha habari katika ukurasa wa mbele wa gazeti rasmi la serikali Rodong Sinmun limeandika kuhusu mkutano kati ya Kim na Trump bila ya kutaja ukweli kwamba viongozi hao wawili wamerejea nyumbani mikono mitupu.
Picha zimemuonesha Kim akizungumza na Trump , mtu ambaye hapo zamani alimshambulia kwa kusema kuwa ni Mmarekani mlemavu wa akili.
"Walikuwa na mazungumzo mazuri na walibadilishana mawazo kuhusiana na masuala halisi yanayotokana na ufunguzi wa enzi mpya ya kuboresha uhusiano kati ya Korea kaskazini na Marekani kwa msingi wa hatua zitakazopigwa ," limeandika gazeti la Rodog.
Korea Kaskazini ilitaka maafikiano
Vyombo vya habari vya taifa havikueleza lolote kuhusiana na kushindwa kwa mazungumzo ama kutokubaliana kuhusiana na madai ya Korea kaskazini ya kufikishwa mwisho vikwazo na miito ya Marekani ya kuharibu kabisa mpango wote wa kinyuklia wa Korea kaskazini.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Korea kaskazini Ri Yong Ho amesema nchi yake ilitoa mapendekezo halisi katika mkutano huo.
Shirika rasmi la habari la Korea kaskazini pia lilichukua msimamo wa mapatano zaidi, likisema Kim ametoa shukrani zake kwa Trump kwa kuwezesha juhudi zenye manufaa na kufanikisha mkutano huo na mazungumzo wakati amefanya safari ndefu na kusema kwaheri, na kuahidi mkutano mwingine.
Vyombo vya habari nchini Japan mshirika wa Marekani vililenga hata hivyo katika kuvunjika kwa mazungumzo hayo pamoja na shaka juu ya hali ya baadaye ya diplomasia ya kinyuklia kutokana na jinsi pande hizo mbili zilivyoshindwa kupunguza mwanya licha ya uhusika wa binafsi wa viongozi hao katika majadiliano.
Washirika wa Marekani wana wasiwasi
Wachambuzi wengi nchini Japan, nchi ambayo mara kwa mara ni lengo la vitisho vya Korea kaskazini , wamekuwa na wasi wasi kwamba Trump anaweza kufikia makubaliano ambayo yataiacha nchi hiyo ambayo ni mkoloni wa zamani wa Korea kaskazini ikiwa katika hali ya kupewa vitisho vya kinyuklia wakati wowote.
Rais wa Korea kusini Moon Jae-In amesema leo kwamba serikali yake ina mipango ya kufanya majadiliano na Marekani kuhusu uwezekano wa kuanzisha miradi ya pamoja ya kiuchumi kati ya Korea kaskazini na Korea kusini kuishawishi nchi hiyo kuachana na mpango wa kinyuklia.
Kim Jong Un ameanza ziara rasmi nchini Vietnam leo baada ya mkutano wake na Trump.