Korea Kaskazini kushinikizwa kuingia mazungumzo ya nyuklia
22 Julai 2021Awali Korea Kaskazini ilisisitiza kuwa haitaingia katika mpango huo kutokana na kile ilichokiita uchokozi au uhasama kutoka kwa Marekani.
Naibu Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Wendy Sherman alikuwa mjini Soul kama sehemu ya ziara yake ya eneo hilo itakayompeleka nchini China mwishoni mwa Juma. Sherman atakuwa afisa wa juu wa Marekani kuitembelea China tangu Rais Joe Biden alipochukua madaraka.
Leo Sherman amekutana na Waziri wa mambo ya kigeni wa Korea Kusini Chung Eui-yong kwa mazungumzo juu ya Korea Kaskazini, Muungano wa kijeshi kati ya Seoul na Marekani na masuala mengine muhimu ya eneo hilo.
Kulingana na taarifa kutoka wizara ya mambo ya nje ya Korea Kusini, wawili hao walikubaliana kuendelea na majadiliano ya karibu kuishawishi Korea Kaskazini, kurejea katika mazungumzo hayo ya nyuklia na kukubaliana kuwa mazungumzo ni muhimu ili kuondoa silaha za nyuklia na kuwa na amani ya kudumu katika Rasi ya Korea.
Katika mkutano wake na Rais Moon Jae In, Wendy Sherman amesema anatumai taifa hilo litaridhia pendekezo la Marekani la kuwa na majadiliano. Amesema angelipenda kuwa na mazungumzo ya ndani zaidi juu ya Korea Kaskazini na maafisa wa China atakapoutembelea mji wa kaskazini mashariki mwa China wa Tianjin siku ya Jumapili.
Kim Jong Un atangaza ushiriano zaidi na China
Lakini huku kukiwa na maswali kuhusu ushawishi wa China kwa Korea Kaskazini, China bado inabakia kuwa mshirika mkubwa wa taifa hilo.
Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un mapema mwezi huu alitangaza kuendelea kuimarisha uhusiano wake na China huku akijaribu kuinasua nchi yake kutokana na janga lililoutikisa uchumi wake.
Diplomasia inayoendelea kutekelezwa na Marekani inayonuiwa kuisimamisha Korea Kaskazini kuendelea na mpango wake wa nyuklia ili kupata faida ya kiuchumi na kisiasa ilikwama kwa takriban miaka miwili na nusu iliyopita.
Kitu muhimu kinachokwamisha mazungumzo hayo ni hatua ya Korea Kaskazini kutaka Marekani kuondoa sera zake ambazo Pyongyang inaziona ni za kiuchokozi na vikwazo ilivyowekewa na Marekani kutokana na hatua yake ya zamani ya majaribio ya kurusha makombora.
Mjumbe wa Marekani atumai kupata jibu zuri kutoka Korea Kaskazini
Mwezi uliopita dadaake rais Kim aliye na ushawishi Kim Yo Jong aliondoa matumaini ya kuanza upya kwa mazungumzo hayo ya nyuklia, akisema mazungumzo hayo yatawavunja moyo.
Wataalamu wanasema huenda Korea Kaskazini ikaona umuhimu wa kurejea katika mazungumzo hayo iwapo hali yake ya kiuchumi kutokana na janga la virusi vya corona itakuwa mbaya zaidi.
Chanzo: afp,reuters