Korea Kaskazini: Makombora yetu mapya, onyo kwa Korea Kusini
26 Julai 2019Kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un amesema makombora mawili yaliyofyatuliwa chini ya uangalizi wake yakifanyiwa majaribio, ni onyo kali kwa Korea kusini kuhusu mipango yake ya kufanya luteka za kijeshi na Marekani.
Majaribio ya makombora yaliyofanywa Alhamisi na Korea Kaskazini, yalikuwa ya kwanza tangu Kim Jong Un na rais wa Marekani Donald Trump walipokutana katika eneo lisilo la kijeshi kati ya Korea ya kusini na kaskazini na kukubaliana kuanza tena mazungumzo kati yao kuhusu silaha za nyuklia.
Makubaliano haya hayajaanza kutekelezwa, na hata kabla ya majaribio ya makombora yaliyofanywa jana, Korea Kaskazini ilishaonya kuwa huenda mazungumzo yakaathiriwa na hatua ya Marekani na Korea Kusini kukataa kuachana na luteka za kijeshi zilizopangwa kufanyika mwezi ujao.
Korea Kaskazini: Makombora yetu mapya ni ya kisasa na yana mfumo wa 'kimkakati'
Bila ya kutoa maelezo zaidi, shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya korea Kaskazini KCNA limetangaza kuwa majaribio ya jana, yalikuwa ya aina ya makombora mapya ya kimkakati yenye mfumo wa kiufundi ya kuyaelekeza na ambayo yalituma onyo kali kwa wachochezi wa vita wa Korea Kusini, kuhusu hatua yao ya kuendelea kukaidi maonyo na kuendelea kufanya luteka za pamoja na Marekani.
Waangalizi wa Korea Kusini wamesema kuwa makombora hayo ya masafa mafupi yaliyofyatuliwa Alhamisi yaliruka umbali wa kati ya kilomita 450 na 700 kabla ya kuanguka baharini kati ya rasi ya Korea na Japan.
Umbali huo unayawezesha makombora hayo kushambulia eneo lolote ndani ya Korea Kusini.
Kuna zaidi ya wanajeshi 30,000 wa Marekani nchini Korea Kusini, na luteka zao za kijeshi ya kila mwaka pamoja na Korea Kusini zimeendelea kuighadhabisha Korea Kaskazini.
Waziri wa ulinzi wa Japan ameutaja ufyatuliaji wa makombora hayo kuwa jambo la kusikitisha mno. Nayo ofisi ya usalama wa kitaifa ya Korea Kusini imeelezea wasiwasi mkubwa huku Marekani ikitaka matendo hayo ya uchokozi yasitishwe.
Kwa mujibu wa KCNA, Kim alisema makombora hayo ya kisasa yanaweza kuruka kilomita chache juu ya usawa wa bahari, hali inayoyafanya kuwa vigumu kuzuiwa. Shirika hilo la habari limeongeza kuwa Kim ameionya Korea Kusini dhidi ya kupuuza onyo hilo.
Pompeo: Mipango ya mazungumzo kuendelea
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo amesema anaamini mipango ya mazungumzo itaendelea na kwamba majaribio hayo mapya ni mkakati wa kuelekea kwenye mazungumzo.
Kwenye mahojiano yake na kituo cha televisheni cha Bloomberg, Pompeo amesema kila mmoja anajaribu kujiandaa kwa mazungumzo na kujenga hali ya usawa na kuweka hali ngumu kwa upande mwingine.
Korea Kaskazini ilifanya majaribio kama hayo ya masafa mafupi mwezi Mei, ambayo Rais Trump alipuuza kuwa ya kawaida.
Majaribio ya hivi karibuni yamejiri baada ya mshauri wa usalama wa Marekani John Bolton kuzungumza na maafisa wakuu wa Korea kusini mjini Seoul.