1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yarusha kombora kwenye Bahari ya Mashariki

28 Septemba 2021

Jeshi la Korea Kusini limesema Korea Kaskazini imerusha kombora moja kuelekea katika Bahari ya Mashariki, huku Korea Kaskazini ikisema hakuna mtu anayeweza kuinyima nchi hiyo haki yake ya kujilinda.

https://p.dw.com/p/40xNV
Nordkorea Raketentest
Picha: Ahn Young-joon/AP Photo/picture alliance

Wakuu wa vikosi vya jeshi vya Korea Kusini pamoja na wizara ya ulinzi ya Japan, wamesema Jumanne kuwa kombora hilo la masafa mafupi limerushwa kutoka jimbo la kaskazini la Jagang linalopakana na China, kuelekea kwenye bahari hiyo inayojulikana pia kama Bahari ya Japan.

Tukio hilo limefanyika siku chache baada ya Kim Yo Jong, dada wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, ambaye ana ushawishi mkubwa, kutangaza kuwa nchi hiyo iko tayari kurudi kwenye meza ya mazungumzo. Hata hivyo, Jong amesema ili hilo kufikiwa inawapasa kuhakikisha kuna hali ya kuheshimiana na kuachana na mitazamo ya kudhaniana vibaya.

Azimio la kumaliza vita

Katika siku za hivi karibuni, Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in alirudia wito wake wa muda mrefu kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutaka kuwepo kwa azimio la kumalizika vita vya Korea hizo mbili kama njia ya kurejesha amani. Korea Kaskazini inakabiliwa na vikwazo kadhaa vya kimataifa kutokana na mipango yake iliyopigwa marufuku ya kutengeneza silaha za nyuklia na makombora.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Korea Kusini, Boo Seung-chan amesema wamesikitishwa na kitendo kilichofanywa leo na Korea Kaskazini, katika wakati ambao ni muhimu sana kuleta utulivu kwenye Rasi ya Korea.

Saa chache baada ya tangazo la kurushwa kombora hilo kutolewa, Balozi wa Korea Kaskazini kwenye Umoja wa Mataifa, Kim Song ameitaka Marekani kuachana na "sera yake ya uhasama" kuelekea nchi hiyo.

 UN Generalversammlung Rede Kim Song
Balozi wa Korea Kaskazini kwenye Umoja wa mataifa, Kim SongPicha: picture-alliance/AP Photo/R. Drew

Akihutubia jana katika Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa, Song amesema hakuna mtu anayeweza kuinyima nchi yake haki ya kujilinda, kutengeneza, kumiliki na kufanya majaribio ya mifumo yake ya silaha ambayo ni sawa na ile ya Korea Kusini pamoja na mshirika wake Marekani.

''Kwa kuzingatia kwamba ushirikiano wa kijeshi wa Korea Kusini na Marekani unaongeza kitisho kwa Korea Kaskazini, hakuna mtu anayeweza kutunyima haki ya kujilinda. Tunatengeneza mifumo yetu ya ulinzi kwa lengo la kujilinda na kwa usalama na amani ya nchi yetu. Kwa kuzingatia kwamba ushirikiano wa kijeshi wa Korea Kusini na Marekani unaongeza kitisho kwa Korea Kaskazini, hakuna mtu anayeweza kutunyima haki ya kujilinda,'' alifafanua Song.

Matumaini ya uhusiano mzuri

Song amesema ana uhakika kwamba matarajio mazuri yatafunguliwa kwenye uhusiano kati ya Marekani na Korea Kaskazini na Korea Kusini, iwapo Marekani itajizuia kuitisha nchi hiyo.

Kwa miaka mingi Korea Kaskazini imekuwa ikitengeneza makombora yenye uwezo sio tu ya kuipiga Korea Kusini na Japan, lakini pia ina vichwa vya nyuklia vya masafa marefu yanayoweza kufika hadi Marekani. Kulingana na takwimu za shirika la Marekani linalohusika na udhibiti wa silaha, kuanzia mwezi Agosti mwaka 2020, Korea Kaskazini ilikuwa na vichwa vya makombora ya nyuklia 30 hadi 40.

Wakati huo huo Marekani imelaani vikali jaribio la kufyatua kombora lililofaywa na Korea Kaskazini, ambalo linasababisha kitisho kwa jirani zake na jumuia ya kimataifa. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imeitaka nchi hiyo kurejea kwenye meza ya mazungumzo ya kuachana na matumizi ya silaha za nyuklia.

(AFP, DPA, AP, Reuters)