1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKorea Kusini

Korea Kaskazini yarusha makombora mawili baharini

25 Julai 2023

Korea Kaskazini imerusha makombora mawili ya masafa mafupi kuelekea baharini, karibu na pwani yake ya mashariki, saa chache baada ya nyambizi ya Marekani yenye silaha za nyuklia kuwasili katika kisiwa cha Jeju.

https://p.dw.com/p/4UKgI
Nordkorea testet erneut Rakete
Urushaji wa kombora la Pyongyang unaonekana ni katika kujibu hatua ya nyambizi ya nyuklia ya Marekani kuwasili Korea Kusini.Picha: KCNA via REUTERS

Vyombo vya habari vya Korea Kusini na Japan vimeeleza Jumanne kuwa makombora hayo yalifyatuliwa Jumatatu na yaliruka umbali wa kilomita 400, kabla ya kuangukia katika Bahari ya Mashariki, ambayo pia inajulikana kama Bahari ya Japan, iliyoko kati ya Rasi ya Korea na Japan. Taarifa ya pamoja ya majeshi ya Korea Kusini na Japan imeeleza kuwa makombora hayo yalirushwa kutoka eneo la karibu na Pyongyang.

Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida amelaani tukio hilo, akisema Korea Kaskazini imekuwa ikirudia mara kwa mara kurusha makombora, ambapo ni kitishio kwa amani na utulivu sio tu wa Japan, lakini pia kanda yote ya jumuia ya kimataifa, na jambo hilo halikubaliki kabisa.

Japan G7 Gipfel in Hiroshima | Premier Fumio
Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida Picha: The Yomiuri Shimbun/AP Photo/picture alliance

''Ufyatuaji wa makombora unakiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Japan tunalaani na kupinga kitendo hicho. Tutaendelea kufanya kila tuwezalo kufuatilia na kushirikiana kiusalama kupitia muungano wa Japan, Marekani na Korea Kusini, kulinda amani na utulivu wa kikanda,'' alisema Kishida wakati akizungumza Jumanne na waandishi habari mjini Tokyo.

Marekani yalaani

Ikulu ya Marekani nayo imelaani hatua ya Korea Kaskazini kurusha makombora hayo, ikiwa ni mara ya tatu kufanya hivyo tangu wiki iliyopita. Hata hivyo, jeshi la Marekani limesema kwamba urushaji huo wa makombora haukuwa na kitisho kwa maafisa wa Marekani, au kwa washirika wa Marekani.

Makombora hayo yamerushwa huku kukiwa na mvutano mkubwa katika Rasi ya Korea wakati ambapo Korea Kusini na Marekani zinajaribu kuongeza ushirikiano wa kijeshi katika kukabiliana na vitisho vinavyoongezeka vya nyuklia vya Korea Kaskazini.

Südkorea Nordkorea testet erneut Rakete
Runinga ya Korea Kusini ikionyesha moja ya kombora lililorushwa na Korea KaskaziniPicha: Ahn Young-joon/AP Photo/picture alliance

Pia yamerushwa saa chache baada jeshi la Korea Kusini kusema kuwa nyambizi ya Marekani yenye silaha za nyuklia imewasili katika kisiwa cha Jeju ambako kuna kambi ya jeshi la mawanamaji ya Korea Kusini.

Wiki iliyopita, Marekani ilipeleka nyambizi yake hiyo katika bandari ya Busan, Korea Kusini kwa mara ya kwanza tangu miaka ya 1980. Korea Kaskazini nayo ikajibu haraka kwa kufanya majaribio ya kurusha makombora mawili.

Korea Kaskazini kuadhimisha 'Siku ya Ushindi'

Wakati huo huo, Korea Kaskazini imerusha makombora hayo kabla ya maadhimisho ya miaka 70 ya makubaliano ya kusitisha mapigano ya mwaka 1953, ambayo yalimaliza uhasama kati ya Korea Kaskazini na Kusini, yatakayofanyika wiki hii.

Inaelezwa kuwa maadhimisho hayo yanayojulikana kama Siku ya Ushindi Kaskazini, yatahusisha pia gwaride la kijeshi katika mji mkuu, Pyongyang, ambapo kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un anaweza kuonyesha makombora yake yenye uwezo wa nyuklia ambayo yametengenezwa kwa ajili ya kuwalengama wapinzani wake wa kikanda pamoja na Marekani.

(AFP, AP, DPA, Reuters)