1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yasema iko tayari kuzungumza na Marekani

25 Mei 2018

Korea Kaskazini yasema bado ipo tayari kuzungumza na Marekani hata baada ya rais Donald Trump kuuvunja mkutano huo wa kilele kati yake na Kim Jong Un.

https://p.dw.com/p/2yJ5n
Südkorea TV Bildschirm Donald Trump, Kim Jong Un
Picha: picture-alliance/AP Images/A. Young-joon

Rais Trump alieleza hapo jana kwamba hatakutana na Kim Jong Un na sababu aliyoitoa ni kuwepo mazingira ya ghadhabu na uhasama wa wazi. Naibu waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini, Kim Kye Gwan amesema nchi yake imesikitishwa na uamuzi huo wa Marekani.

Mkutano huo ulionekana kama fursa ya kihistoria kwa Marekani kuweza kuishawishi Korea Kaskazini kuacha mpango wake wa silaha za nyuklia na siku ya Alhamisi, waandishi wa habari wa kimataifa walishuhudia Korea Kaskazini ilipokifunga kituo chake kikuu cha kufanyia majaribio ya nyuklia.

Wakati Korea Kaskazini ilipotoa kauli kali dhidi ya makamu wa rais wa Marekani Mike Pence na mshauri wa masuala ya usalama wa Rais Trump, John Bolton, kauli hiyo ndio ilikuwa sababu ya Trump kuuvunja mkutano huo wa kilele kati yake na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un.

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong UnPicha: picture-alliance/Yonhap

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameelezea wasiwasi mkubwa juu ya kuvunjika kwa mkutano huo na wakati huo huo amezihimiza pande zote kuendelea kuzungumza.

China imezitaka Marekani na Korea Kaskazini kuonyesha subira na kutafuta maridhiano. Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje wa China, Lu Kang amebainisha kuwa licha ya Trump kuuvunja mkutano huo lakini amesema yupo tayari kukutana na Kim Jong Un baadaye.

Rais wa China Xi Jinping
Rais wa China Xi JinpingPicha: Reuters/J. Lee

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amesema anatumai juhudi za kuondoa silaha za nyuklia kwenye rasi ya Korea zitaendelea.   Lengo la mkutano baina ya Trump na Kim Jong Un lilikuwa kuondoa hatari inayotokana na silaha za nyuklia za Korea Kaskazini. Trump amesema kutofanyika mkutano huo wa kilele ni pigo kubwa kwa Korea Kaskazini na dunia kwa jumla.

Japan imesema itaendelea kuwa na ushirikiano wa karibu na Marekani na Korea Kusini. Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in ameelezea wasiwasi wake kwamba mkutano huo hautafanyika na amehimiza nchi zote mbili kutafuta mazungumzo ya moja kwa moja. Rais Trump aliwekeza mno katika mafanikio ya mkutano huo uliopangwa kufanyika nchini Singapore, lakini kila tarehe ilipokaribia ndipo matarajio kati ya pande hizo mbili yalipozidi kudidimia.

Marekani imesema wazi kuwa inataka kuona Korea Kaskazini haimiliki silaha zozote za nyuklia lakini Korea kaskazini nayo imeapa kuwa haitoachana na mpango wake wa nyuklia hadi pale itakapohisi kwamba iko salama kutokana na kile ilichokitaja kuwa ni unyanyasaji wa Marekani.

Mwandishi:Zainab Aziz/RTRE/AFPE/p.dw.com/p/2yI0v

Mhariri:Grace Patricia Kabogo