1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yasema itazindua silaha mpya ya kimkakati

Zainab Aziz Mhariri: Bruce Amani
2 Januari 2020

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amesema majaribio hayo mapya yataliimarisha kiufundi jeshi la Korea Kaskazini. Matamshi hayo ya Kim Jong Un yamezusha wasiwasi mkubwa.

https://p.dw.com/p/3Vaqr
Nordkorea 2017 | Militärparade in Pjöngjang
Picha: picture-alliance/AP Photo/Wong Maye-E

Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya teknolojia hatua hiyo ya Korea Kaskazini inaweza kuiwezesha nchi hiyo kuunda makombora ya masafa tofauti na pia silaha za nyuklia. Lee Sang Meen msemaji wa wizara ya Korea Kusini inayohusika na masuala ya uhusiano mwema kati ya nchi hiyo na Korea kaskazini amesema jitihada za kuiwezesha Korea Kaskazini kuachana na mpango wake wa nyuklia zitakuwa hazileti faida yoyote ikiwa Korea Kaskazini itachukua hatua ya kuanzisha kile inachosema kuwa ni silaha ya mkakati mpya.

Meen amesema serikali ya Korea Kusini inaweka wazi kwamba ikiwa upande wa Kaskazini utafanya majaribio ya silaha yake mpya, basi mazungumzo ya kuiwezesha Korea kaskazini kuachana na mpango wake wa nyuklia hayatafanikiwa na juhudi za kuleta amani katika Rasi ya Korea hazitazaa matunda. 

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong UnPicha: picture-alliance/AP Photo/Korean Central News Agency/Korea News Service

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea wasiwasi wake kutokana na tamko la Korea Kaskazini kwamba inaweza kuanza tena mpango wake wa nyuklia na makombora ya masafa marefu na majaribio ya makombora. Guterres anatarajia kuwa Korea Kaskazini haitafanya majaribio hayo na kwamba itazingatia maazimio ya Baraza la Usalama yanayosisitiza kutokuendelea na utengenezaji wa silaha za nyuklia duniani. Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa amesema ushirikiano wa kidiplomasia ndio njia pekee endelevu itakayoleta amani.

Rais wa Marekani Donald Trump ambaye mnamo mwaka 2018 alikua kiongozi wa kwanza wa Marekani kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini amesema Kim Jong Un alitia saini makubaliano ya kuachana na mpango wa nyuklia na kwamba anaamini kuwa kiongozi huyo wa Korea Kaskazini hatakiuka ahadi yake.

Kwa upande wake kiongozi wa Korea Kkaskazini Kim Jong Un amelalamika kwamba Marekani imeendelea kufanya luteka za kijeshi pamoja na Korea Kusini, imeendelea kutumia silaha kali na kuiwekea vikwazo nchi yake huku ikidai hatua chungunzima zichukuliwe kwa njia za kibabe.

Mwezi uliopita, Korea kaskazini iliionya Marekani na kuipa hadi mwisho wa mwaka jana kupendekeza makubaliano mpya kuhusu mazungumzo ya silaha za nyuklia za Korea Kaskazini.

Wachambuzi wanasema tamko la Kim Jong Un ni ishara kuwa Korea Kaskazini inaweza kufanya tena majaribio mengine makubwa baada ya kusitisha kufanya majaribio ya makombora kwa zaidi ya miaka miwili katika harakati za kumaliza mzozo wa kidiplomasia na Marekani.

Vyanzo:RTRE/p.dw.com/p/3VZYU