Korea Kaskazini yatishia kuufuta mkutano na Marekani
16 Mei 2018Awali, Korea Kaskazini iliufuta pia mkutano wa ngazi ya juu ambao ungefanyika leo kati yake na Korea Kusini.
Onyo hilo la Korea Kaskazini limetolewa na makamu wa kwanza wa waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, katika kipindi cha masaa kadhaa baada ya taifa hilo kusitisha ghafla mkutano wa maafisa wa ngazi ya juu na Korea Kusini, ikipinga mazoezi ya kijeshi ya pamoja kati ya Marekani na Korea Kusini, ambayo kwa muda mrefu serikali ya Pyongyang imekuwa ikidai ni maandalizi ya uvamizi.
Hatua ya kuondosha hofu
Hatua hiyo ya kushtukiza inapoza joto la hatua zisizo za kawaida za kuridhia mazungumzo kutoka taifa hilo ambalo kwa mwaka uliopita lilikuwa likifanya mfululizo wa majaribio ya makambora,na kuzua wasiwasi kwamba eneo hilo lipo katika hatua ya kuingia vitani. Wachambuzi wanasema sio kwamba Korea Kaskanzini inataka kupingana na hatua zote za kidiplomasia lakini inataka kunufaika katika mazungumzo hayo kati ya kiongozi Kim na Rais Trump,iliyopangwa Juni 12 huko Singapore.
Katika taarifa yake iliyotangazwa na vyombo vya habari vya umma vya nchi hiyo makamu wa kwanza wa wizara ya mambo ya nje wa Korea Kaskanzini, Kim Kye Gwan amenukuliwa akisema "Hatuna tena maslahi katika mazungumzo ambayo yanatatuweka katika wakati mgumu na kufanikisha matakwa ya upande mmoja, ambayo itatulazimisha kulizingatia pale tutakapo ridhia mkutano wa kilele kati ya Korea Kaskazini na Marekani.
Mshauri wa Trump akosolewa
Aidha katika taarifa yake hiyo ameyakosoa kauli ya mshauri wa masuala ya usalama wa Trump, John Bolton, na maafisa wengine ambao walisema Korea Kaskazini wanapaswa kufuata namna ya Libya iachane na shughuli zake za kinyuklia , sawa na ilivyofanyika wakati wa Utawala wa kiongozi wa wakati huo Muammar Gaddafi. Na kutoa ushahidi wa utekelezaji wa hatua hiyo. Pia aligusia suala la maoni ya Marekani kwamba taifa lao linapaswa kuachana kabisa uundaji wa silaha za kibiolojia na kikemikali.
Baadhi ya wachambuzi wanasema kulizusha suala la Libya, ambayo iliiharibu mpango wake wa nyuklia katika miaka ya 2000 kwa masharti ya kupunguziwa vikwazo iliyokewa katika kipindi hicho inaweza kuhatarisha mustakabali wa mazungumzo hayo kati ya Korea Kaskazini na Marekani. Kim Jong Un aliingia madarakani majuma kadhaa baada ya kifo cha kiongozi wa zamani wa Libya Moammar Gadhafi kilichotokea katika mikono ya vikosi vya waasi Oktoba 2011.
Mwandishi: Sudi Mnette/APE
Mhariri: Gakuba, Daniel