1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yawekewa vikwazo vipya

Josephat Charo
12 Septemba 2017

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeiwekea vikwazo vipya Korea Kaskazini, ikiweka marufuku ya uuzaji wa nguo katika nchi za kigeni na kudhibiti usafirishaji wa bidhaa za mafuta.

https://p.dw.com/p/2jllT
New York UN Sicherheitsrat Nordkorea Sitzung
Picha: picture-alliance/Photoshot/L. Muzi

Likiungwa mkono na China na Urusi baraza hilo lenye nchi 15 wanachama limepiga kura kwa kauli moja kuridhia vikwazo vilivyoandaliwa na Marekani, mwezi mmoja baada ya kupiga marufuku makaa ya mawe, madini ya risasi na vyakula vya baharini, kufuatia hatua ya Korea Kaskazini kufyetua kombora la masafa marefu linaloweza kuvuka mabara.

Vikwazo hivyo vipya vinaipiga marufuku Korea Kaskazini kuagiza gesi asilia kutoka nje. Azimio hilo nambari 2375 la mwaka 2017 linapiga marufuku uuzaji wa nguo katika nchi za nje na linaipiga marufuku nchi yoyote kuamuru vibali vipya kwa wafanyakazi wa Korea Kaskazini - vyanzo viwili muhimu vya fedha taslimu kwa taifa hilo la kaskazini mashariki mwa Asia.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley ameliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba vikwazo vipya vilivyopitishwa ni vikali zaidi kuwahi kuwekewa Korea Kaskazini. "Leo tunasema ulimwengu katu hautakubali Korea Kaskazini iliyojihami silaha za nyuklia. Na leo baraza la usalama linasema ikiwa utawala wa Korea Kaskazini hauwezi kuukomesha mpango wake wa nyuklia, tutachukua hatua kuizuia sisi wenyewe."

Haley amesisitiza kwamba hatua hizi hufanya kazi tu iwapo mataifa yote yatazitekeleza kikamilifu na kwa hima. Amedokeza kuwa baraza la usalama limechoka kuubembeleza utawala wa Pyongyang kufanya kitu kilicho sahihi, badala yake jumuiya ya kimataifa inachukua hatua kuizuia Korea Kaskazini isifanye kitu kisichofaa. Hata hivyo Haley amesisitiza kwamba Marekani haitaki vita na iwapo Korea Kaskazini itaachana na mpango wake wa nyuklia na kuthibitisha inaweza kuishi kwa amani, basi ulimwengu utaishi nayo kwa amani.

USA UN-Sicherheitsrat in New York - US-Botschafterin Nikki Haley
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki HaleyPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Matthews

Makubaliano ya mwisho yaliafikiwa baada ya mashauriano kati ya Marekani na China, mshirika mkubwa wa kibiashara wa Korea Kaskazini. Haley amesifu uhusiano imara kati ya rais wa Marekani, Donald Trump, na rais wa China, Xi Jinping, kama kipengee muhimu katika kupitishwa kwa azimio hilo.

China yahimiza mdahalo

Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa, Liu Jieyi, ameitaka Korea Kaskazini iliheshimu azimio hilo na kuzitolea wito pande zote husika kuwa na utulivu. "China inaihimiza Korea Kaskazini kuzingatia kwa makini matarajio na ari ya jumuiya ya kimataifa, isitishe mpango wake wa nyuklia na utengenezaji wa makombora. Iheshimu maazimio ya baraza la usalama, isifanye tena majaribio zaidi ya silaha za nyuklia na makombora na irejee katika mkondo wa kuangamiza silaha zake za nyuklia."

China imeitaka Marekani iache kuitenga Korea Kaskazini na irejee katika meza ya mazungumzo na kusuluhisha masuala yatakayosaidia kusitisha au kukomesha kabisa mipango ya nyuklia ya Korea Kaskazini na kuhakikisha amani ya kudumu katika rasi ya Korea.

Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe amelisifu pendekezo hilo. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Tokyo Abe amedokeza kwamba nchi yake inataka kudhihirisha uongozi kuleta mageuzi katika sera za Korea Kaskazini kupitia ushirikiano wa karibu na jumuiya ya kimataifa. "Napongeza sana kuridhiwa kwa haraka kwa azimio hili la vikwazo vikali dhidi ya Korea Kaskazini. Nadhani jumuiya ya kimataifa inatakiwa kulitekeleza kikamilifu azimio hili. Ni muhimu kuendelea kuishinikiza Korea Kaskazini kuifanya ibadili sera zake."

Korea Kusini imesema vikwazo vipya ni onyo kali kwa utawala wa Pyongyang kutoka wa jumuiya ya kimataifa kwamba uchokozi usiokoma huongeza hali ya kutengwa na shinikizo la kiuchumi. Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Korea Kusini imesema serikali mjini Seoul itaendelea kuimarisha mahusiano na jumuiya ya kimataifa kuhakikisha azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatekelezwa kikamilifu. Taarifa ya wizara hiyo imesema Korea Kusini itapania kuangamiza silaha za nyuklia za Korea Kaskazini na kuleta amani ya kudumu katika rasi ya Korea.

Mwandishi:Josephat Charo/afpe/rtre/ape

Mhariri: Bruce Amani