Korea Kusini yajipanga kumkaribisha Kim Jong Un
26 Aprili 2018Kwa pamoja, viongozi hao wawili watapanda mti wa kumbukumbu wakitumia udongo wa milima na maji ya mito kutoka nchi zote mbili, mara tu baada ya Kim kuvuuka mpaka kesho Ijumaa, saa tatu asubuhi kwa majira ya Korea.
Mkuu wa utumishi katika Ikulu ya Korea Kusini, Im Jong-seok, amewaambia waandishi wa habari kwamba mti watakaoupanda viongozi hao ni aina ya msindano, ambao ni mti unaopendwa na watu wa Korea zote mbili, na chini yake utawekwa kibao kilichoandikwa "Amani na Maendeleo Huatikwa" na sahihi za viongozi hao wawili.
Ratiba inaonesha kuwa Moon atampokea Kim baada ya kuvuuka kuta za kangiriti ambazo zinaunda kile kinachoitwa mstari wa utengano mpakani mwa nchi zao, na kisha wawili hao wataongozana kwa miguu kwa muda wa dakika 10, kuelekea kwenye uwanja kwa ajili ya kuangalia gwaride la heshima ya kijeshi la Korea Kusini.
Hii ni kwa mujibu wa maafisa wa serikali ya Korea Kusini hivi leo, wakati wakitangaza ratiba ya ziara hii ya kihistoria, ambayo inatajwa kuwa kama ishara ya kufunguka kwa milango ya maelewano baada ya zaidi ya nusu karne ya uhasama baina yao.
Mkutano wa kilele wa Kim na Moon utafanyika kwenye kijiji cha Panmunjom, ukitazamiwa kujikita kwenye mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini, ingawa pia panatarajiwa kufanyika shughuli nyengine nyingi za kuimarisha mahusiano mapya yanayochipua, wakati Kim akiwa kiongozi wa kwanza wa Korea Kaskazini kuvuuka mpaka tangu kumalizika kwa Vita vya Korea vilivyopiganwa kuanzia mwaka 1950 hadi 1953.
Ziara yenye ujumbe mzito
Kwenye ziara hii ya aina yake, Kim anasindikizwa na maafisa wa ngazi za juu wa Korea Kaskazini, akiwemo dada yake mwenye ushawishi mkubwa, Kim Yo Jong, ambaye mnamo mwezi Februari aliongoza ujumbe wa nchi yake kwenye Michezo ya Olimpiki ya Pyeongchang nchini Korea Kusini, kitendo kinachotajwa kuwa cha kwanza cha waziwazi kufungua upya mawasiliano ya Korea Kaskazini.
Mkewe Kim Jong Un, Ri Sol Ju, atahudhuria pia sehemu za mkutano wa kesho wa kilele, ingawa hadi sasa haijawa wazi ni maeneo yapi mahsusi atakayoshirikishwa.
Vile vile, haijafahamika endapo viongozi hao wawili watatangaza matokeo ya mkutano wao kwa waandishi wa habari baada ya vikao kumalizika, ingawa inaeleweka kuwa sehemu ngumu zaidi ya mazungumzo haya ni kiwango cha ukubalifu wa Korea Kaskazini kwenye kujiondoa katika mpango wa nyuklia.
Mkutano wa kesho wa kilele na mkutano mwengine uliopangwa kufanyika kati ya Kim na Rais Donald Trump wa Marekani mwishoni mwa mwezi ujao au mwanzoni mwa Juni, ilipangwa baada ya uamuzi wa ghafla wa Kim kuelezea utayarifu wake wa kukubali majadiliano kuhusiana na mpango wake wa nyuklia, baada ya mwaka mzima wa majaribio ya makombora na silaha za nyuklia.
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman