Korea kusini yaonesha hofu ya silaha za Korea kaskazini
11 Oktoba 2020Silaha za Korea kaskazini zilizooneshwa ni makombora mapya ya masafa marefu katika gwaride la kijeshi
Wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 75 tangu kuasisiwa chama tawala mjini Pyongyang jana Jumamosi, Korea kaskazini ilionesha aina mbali mbali za mifumo ya silaha, ikiwa ni pamoja na makombora mawili ambayo yameoneshwa hadharani kwa mara ya kwanza kwa mataifa ya nje.
Moja ni lile ambalo lilionekana kama kombora la masafa marefu linaloweza kufika katika bara jingine ambalo ni kubwa kuliko kombora lolote la Korea kaskazini linalofahamika la masafa marefu linalofika katika bara jingine, ICBM, na lingine linaonekana kama ni aina iliyofanyiwa mabadiliko ambalo linaweza kufyatuliwa kutoka katika nyambizi.
Wakati baadhi ya wataalamu wanasema inaweza kuwa ni makombora ya mfano tu ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi, kuoneshwa kwao hadharani kunaonesha kuwa Korea kaskazini imekuwa ikiendelea kusogea mbele katika kuimarisha uwezo wake wa silaha huku kukiwa na mkwamo katika diplomasia ya nyuklia na Marekani.
Wizara ya ulinzi ya Korea kusini imesema leo inaeleza wasi wasi wake juu ya ukweli kwamba "Korea kaskazini imeonesha silaha ikiwa ni pamoja na zile zilizokuwa zinashukiwa kuwa makombora mapya ya masafa marefu." Taarifa ya wizara iliitaka Korea kaskazini kuendelea kuwa sehemu ya makubaliano ya pamoja ya Korea ya mwaka 2018 yenye lengo la kupunguza uadui baina yao.
Mazungumzo ya kinyuklia
Wizara ya mambo ya kigeni ya Korea kusini imetoa taarifa tofauti inayoitaka Korea kaskazini kurejea katika mazungumzo ili kupata kupiga hatua katika nia yake thabiti ya kufikia kutokuwa na silaha za kinyuklia na amani katika rasi ya Korea.
Baada ya mkutano wa dharura wa baraza la usalama la taifa, wajumbe wa baraza hilo nchini Korea kusini walisema wataendelea na kufanya tathmini ya umuhimu wa mkakati wa mfumo wa silaha wa Korea kaskazini uliooneshwa jana na kufanya mapitio mapya ya uwezo wa ulinzi wa Korea kusini.
Mahusiano kati ya Korea mbili yanaendelea kuwa mabaya huku kukiwa na mkwamo wa diplomasia ya kinyuklia kati ya Pyongyang na Washington.
Katika hotuba iliyotolewa wakati wa gwaride hilo la kijeshi, kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un alionya kwamba atatumia uwezo wake wote wa kinyuklia iwapo atatishiwa lakini aliepuka kuikosoa moja Marekani.
Ukweli kwamba Kim anaendelea na hatua alizoziweka binafsi za kuzuwia majaribio ya makombora ya masafa marefu ya kinyuklia bado anataka kuweka nafasi za kidiplomasia hai na Marekani . Lakini baadhi ya wataalamu wanasema atafanya jaribio kubwa la silaha baada ya uchaguzi wa rais wa Marekani hapo Novemba kuimarisha nafasi yake katika majadiliano mapya na Marekani , kwa yeyote atakayeshinda uchaguzi.