Korea Kusini kutobadilishana taarifa za kijasusi na Japan
22 Agosti 2019Ofisi ya rais wa Korea Kusini imesema Alhamisi kuwa nchi hiyo itasitisha hatua hiyo ya kupeana taarifa za kijasusi na Japan tofauti baina ya nchi hizo kuhusu kuhusiana na historia na biashara zikizidi kuongezeka.
Kubadilishana habari za kijeshi sio "maslahi ya kitaifa" kutokana na "mabadiliko makubwa" katika ushirikiano wa kiusalama uliotokana na uamuzi wa Japan kuondoa hadhi ya Korea Kusini ya uuzaji bidhaa nje kwa haraka, amesema Kim You-geun,naibu mkurugenzi wa baraza la kitaifa la usalama la Korea Kusini.
Makubaliano hayo ya taarifa za kijeshi ya miaka mitatu yalikuwa yaanzishwe upya siku ya Jumamosi iwapo kusingekuwepo pingamizi la upande wowote.
Majibu ya Korea Kusini yanatolewa baada ya Japan mapema mwezi huu kutaja sababu za usalama wa kitaifa kuiondoa Korea Kusini kutoka kwa orodha ya mataifa yanayopata kipaumbele cha udhibiti wa bidhaa zinazouzwa nje. Korea Kusini ilijibu kwa kuifutia pia Japan hadhi maalumu ya kibiashara.
Kuondolewa kwa Korea Kusini kutoka kwa orodha hiyo ya mataifa yaliopewa kipaombele ni kutokana na hatua ya kulipiza kisasi kuhusiana na uamuzi wa mahakama ya Korea Kusini mwaka jana kwamba kampuni za Japan zinapaswa kuwafidia wafanyikazi wa Korea Kusini waliolazimishwa kufanya kazi kabla na wakati wa vita vya pili.
Japan inasema masuala ya wakati wa vita yalisuluhishwa katika mkataba wa mwaka 1965 wa kuwianisha uhusiano wa kibiashara lakini mizozo ya kimipaka imesalia katika baadhi ya visiwa.
Mzozo unaokithiri kati ya Korea Kusini na Japan unawakilisha kusambaratika kwa juhudi za Marekani za kuwaunganisha wandani wake wa bara Asia wakati ambapo Marekani iko katika mzozo wa kibiashara na China na kunuia kuanzisha upya mashauriano ya Korea Kaskazini kuondoa mpango wake wa silaha za kinyuklia.