1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea mbili zafanya mkutano wa kihistoria

30 Aprili 2018

Viongozi wa Korea Kaskazini na Korea Kusini wamefanya mkutano wa kilele na ambao ni wa kihistoria katika eneo la mpakani lisilo na shughuli za kijeshi, huku wakiahidi kutafuta amani baada ya miongo mingi ya uhasama

https://p.dw.com/p/2wlv9
Innerkoreanischer Gipfel
Picha: Korea Summit

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un na Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in walipeana mikono katika eneo la mstari wa kijeshi ambao unazitenganisha nchi zao, katika ishara yenye ujumbe mkubwa)).

Kim alimwambia Moon huku akitabasamu kuwa ana furaha kukutana naye, kabla ya mgeni huyo kuvuka upande wa Korea Kusini, na hivyo kuwa kiongozi wa kwanza wa Korea Kaskazini kukanyaga ardhi ya Kusini tangu kumazilika vita vya Korea miaka 65 iliyopita.

Kutokana na mwaliko wa ghafla wa Kim, viongozi hao wawili walivuka na kuingia upande wa Kaskazini huku wakiwa wameshikana mikono kabla ya kuingia katika Jumba la Amani katika upande wa Kusini wa kijiji cha Panmunjom kwa ajili ya mkutano wao wa kilele -- ambao ni wa tatu wa aina hiyo tangu uhasama ulipositishwa mwaka wa 1953.

Kim alikanyaga ardhi ya Korea Kusini
Kim alikanyaga ardhi ya Korea KusiniPicha: KOCIS

Kim, ambaye utawala wake unatuhumiwa kwa ukiukaji wa haki za binaadamu, alimwambia Moon kuwa mkutano huo ni mwanzo wa historia mpya. "Nnataka kusema kuwa tunapaswa kujitahidi ili tukiangalia nyuma katika miaka 10 iliyopita na kusema kuwa haikupotea tu. Natumai kuwa tunaweza kukutana mara kwa mara ili kutatua matatizo baina ya nchi zetu".

Naye aliitaja hatua ya kihistoria ya Kim kuvuka mstari wa kijeshi kuwa ya "ujasiri” na "ishara ya Amani” na akasema anatumai watashirikiana pamoja ili kufanya "maamuzi ya ujasiri”. "Natumai kuwa tunaweza kuwa na mazungumzo yenye matokeo makubwa na kufikia makubaliano, ili tuwape zawadi kubwa raia wetu na kila mmoja kote duniani, wanaotaraji kupata Amani"

Kim aliandamana na dada yake na mshuauri wa karibu Kim Yo Jong na kiongozi wa Kaskazini wa mahusiano ya Korea mbili, wakati Moon akiandamana na mkuu wa ujasusi na mkuu wa jeshi.

Mkutano huo wa kihistoria umekuja wiki chache tu kabla ya Kim kukutana na Rais wa Marekani Donald Trump ili kujadili suala la kuondoa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea.

Korea-Gipfel
Kim na Moon walipeana mikono kabla ya mkutanoPicha: Reuters/Korea Summit Press Pool

Afisa wa Korea Kusini amesema Kim na Moon walijadili kuhusu mpango wa kuondoa silaha za nyuklia na kupatikana amani ya kudumu katika rasi ya Korea wakati wa kikao chao cha asubuhi, na wanatarajiwa kusaini tamko la pamoja baada ya kukutana tena leo mchana.

Baada ya mazungumzo hayo ya karibu dakika 90, Kim alirudishwa katika upande wa Kaskazini chini ya ulinzi mkali. Baada ya chakula cha mchana, viongozi hao wawili walipanda mti wa kumbukumbu kabla ya kuanza tena mazungumzo yao, watakayomaliza jioni na chakula cha mchana na kutizama filamu. Wake za marais hao wanatarajiwa kujumuika nao kwa chakula cha jioni.

Marekani ina matumaini kuwa mazungumzo hayo yatapiga hatua katika kupatikana Amani na ustawi. Ikuu ya White House imesema inataraji kuendeleza mazngumzo na Korea Kusini katika matayarisho ya mkutano unaopangwa wa Rais Donald Trump na Kim katika wiki chache zijazo. Trump amesema kuwa anatafakari kuhusu tarehe na mahali pa kuandaliwa mkutano huo.

Mwandishi: Bruce Amani/reuters
Mhariri: Gakuba, Daniel