1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea mbili zakubali kufungua tena njia za mawasiliano

3 Januari 2018

Korea Kaskazini imefungua tena mawasiliano ya mpakani na Korea Kusini, saa kadhaa baada ya rais wa Marekani Donald Trump kumdhihaki kiongozi wa Korea kaskazini kuhusu kitufe chake cha nyuklia.

https://p.dw.com/p/2qG6R
Nordkorea Südkorea Kommunikationskanal in Panmunjom
Picha: picture-alliance/Yonhapnews/Agency

Tangazo la kushtukiza la Korea Kaskazini, lililosomwa kupitia Televisheni ya taifa lilikuja siku moja baada ya serikali mjini Seoul kupendekeza mazungumzo ya ngazi ya juu wakati ambapo mkwamo unaendelea kati ya mataifa hayo kuhusiana na mpango wa makombora ya nyuklia ya Korea Kaskazini.

Hilo pia lilifuatia hotuba ya mwaka mpya ya Kim, ambamo alisema alikuwa tayari kuzungumza na Seoul na atazingatia kutuma ujumbe wa washiriki katika michezo ya majira ya olimpiki ya majira ya baridi itakayofanyika umbali mdogo kutoka mpakani katika kijiji cha Pyeongchang mwezi Februari.

Kim alitoa amri ya kufungua tena njia ya mawasiliano na Korea Kusini katika kijiji cha mapatano cha Panmunjom usiku wa kuamkia Jumatano, alisema afisa wa Korea Kaskazini Ri Son Gwon.

Msemaji wa wizara ya masuala ya muungano ya Korea Kusini Baik Tay-hyun alisema uamuzi huo wa Pyongyang ni muhimu kwa sababu utawezesha kuwepo na mawasiliano ya mara kwa mara kati ya Korea mbili.

Südkorea Nordkorea Kommunikationskanal
Afisa wa Korea Kusini akikagua laini ya simu ya mawasiliano kati ya Korea mbili katika kijiji cha Panmunjom, Januari 3, 2018.Picha: picture-alliance/Yonhapnews/Agency

"Tutajadiliana kuhusu masuala ya utendaji kuhusiana na pendelezo la jana la kufanyika mazungumzo ya Kusini na Kaskazini," alisema Tay-hyun katika mkutano na waandishi wa habari mjini Seoul.

Onyo kali kwa Marekani

Lakini ujumbe wa Kim wa mwaka mpya ulihusisha pia onyo kali kwa Marekani kwamba ana kitufe cha nyuklia mezani kwake, ambalo lilifuatiwa na majibu ya hasira kutoka kwa rais Donald Trump kupitia Twitter, akisema yeye pia anacho kitufe cha nyuklia ambacho ni kikubwa zaidi na chenye nguvu zaidi kuliko cha Kim.

Matamshi ya Trump yalikuja baada ya balozi wake katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley kupuuza pendekezo la mazungumzo kutoka Korea Kusini, akilitaja kuwa suluhu ya muda tu na isiyoridhisha.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Hearther Nauert, pia alionya kuwa huenda Kim anajaribu kusababisha mgawanyiko kati ya Marekani na Korea Kusini.

Kim akaribisha Seoul kukubali pendekezo lake

Lakini kurejesheana mawasiliano kati ya Korea mbili kulionekana kwenda vyema, huku Kim akikaribisha hatua ya Seoul kuunga mkono mapendekezo yake, kwa mujibu wa Ri Son-gwon, ambaye ndiye kiongozi wa idara inayoshughulikia masuala yanayohusu Korea mbili.

Südkorea Panmunjom DMZ Grenze zu Nordkorea
Wanajeshi wa Korea Kusini na Marekani walitoa ulinzi wakati wa tukio la kukumbuka miaka 64 tangu kusainiwa kwa mapatano ya kusitisha vita kati ya Korea mbili, Julai 27, 2017 katika eneo la pamoja la usalama katika kijiji cha Panmunjom.Picha: Getty Images/J. Heon-Kyun

Nchi hizo mbili, zinazotenganishwa na ukanda usiyo na shughuli za kijeshi tangu kumalizika kwa vita vya Korea vya mwaka 1950-1953, zilifanya mazungumzo ya ngazi ya juu kwa mara ya mwisho mwaka 2015 kujaribu kupunguza mzozo.

Laini ya mawasiliano ya simu iliyoko katika kijiji cha mapatano ya kusitisha vita cha Panmunjom, iliendelea kufanya kazi hadi Februari 2016, ambapo maafisa kutoka mataifa yote walikuwa wanaikagua mara mbili kila siku.

Laini hiyo ilifungwa baada ya uhusiano kuporomoka kuhusiana na mgogoro uliohusisha eneo la viwanda la Kaesong, lililokuwa linaedeshwa kwa pamoja kati ya Korea mbili.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre.

Mhariri: Daniel Gakuba