1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuaminika kwa uchaguzi ujao Nigeria mashakani

Mohamed Dahman23 Februari 2007

Imani katika uchaguzi mkuu wa Nigeria inapunguwa kutokana na ishara kwamba Rais Olusegun Obasanjo anatumia hila kwa mchakato huo ili kumweka kibaraka madarakani.

https://p.dw.com/p/CHJQ
Rais Olesegun Obasanjo wa Nigeria lawamani kwa kutaka kupanga matokeo ya uchaguzi mkuu
Rais Olesegun Obasanjo wa Nigeria lawamani kwa kutaka kupanga matokeo ya uchaguzi mkuuPicha: dpa

Taifa hilo lenye kuzalisha mafuta kwa wingi kabisa barani Afrika limeshuhudia kufanya kazi kwa demokrasia kwa kipindi kirefu chini ya utawala wa Obasanjo na uchaguzi huo wa mwezi wa April unapaswa kuadhimisha makabidhiano ya kwanza ya madaraka kutoka kwa kiongozi mmoja aliechaguliwa na wananchi kushika madaraka hadi kwa kiongozi mwengine katika historia yake ya miaka 47 tokea ijipatiea uhuru wake.

Obasanjo ameahidi kufanyika uchaguzi huru na wa haki lakini wanadiplomasia wanasema mtawala huyo wa kijeshi wa zamani anatumia vibaya madaraka yake kuwaondowa wagombea wa upinzani wasishiriki uchaguzi huo,kukwamisha maandalizi ya uchaguzi huo na kukiburuza chama tawala kumuunga mkono mgombea asiejulikana.

Msaidizi waziri wa mambo ya nje wa zamani wa Marekani kwa masuala ya Afrika Herman Cohen ameliambia gazeti la Kimataifa la Herald Tribune kwamba wakati Obasanjo akiingia katika miezi ya mwisho ya kipindi chake cha pili cha miaka minne amekuwa akivuruga demokrasia dhaifu ya nchi yake ili arefushe madaraka yake binafsi.

Maoni ya Cohen yanakubaliwa na baadhi ya wanadiplomasia waandamizi wa mataifa ya magharibi walioko Abuja juu ya kwamba wamekuwa waangalifu katika taarifa zao hadharani kuelezea kuunga mkono uchaguzi huru na kusisitiza umuhimu wa tarehe 29 mwezi wa Mei siku ya kukabidhiana madaraka.Wanadiplomasia hao wamekataa kutajwa majina yao.

Katiba ya Nigeria inampiga marufuku mtu yoyote yule anaekabiliwa na madai ya hujuma na jopo la uchunguzi la serikali kugombania urais au ugavana wa majimbo.

Wiki iliopita Tume Huru ya Uchaguzi ya Taifa ambayo upinzani unaituhumu kuwa inakipendelea chama tawala imesema itawazuwiya madarzeni ya watu wengi wao wakiwa wagombea wa upinzani kwa hoja ya kuhusishwa na rushwa na jopo hilo la serikali.

Orodha ya mwisho ya wagombea wanaodaiwa kuhusika na rushwa haikutolewa bado lakini Makamo Rais Atiku Abubakar ambaye anagombania urais kwa tiketi ya upinzani baada ya chama tawala kumtimuwa tayari ameshtakiwa na jopo hilo linaloundwa na mawaziri wa serikali ya Obasanjo.

Polisi wa kupambana na hujuma wiki iliopita ilianza uchunguzi ndani ya Tume Huru ya Uchaguzi ya taifa kwa watuhumiwa wanaounga mkono upinzani kutoka na kuwepo kwa repoti kwamba wanapinga kuzuiliwa kwa Abubakar kugombania wadhifa wa urais.

Wapiga kura pia wamezusha masuali juu ya uhalali wa uchaguzi huo unaokuja,Mchakato wake umekuwa ukikwamishwa na uhaba mkubwa mno wa mashine za kuandikisha wapiga kura na upinzani umekuwa ukimshutumu Obasanjo kwa kuhusika na hilo.

Mwandiplomasia mmoja mwandamizi wa mataifa ya magharibi aliekataa kutajwa jina lake kwa kuhofia kufukuzwa kutoka Nigeria amesema hali inazidi kuwa mbaya kila uchao kwamba wanafanya hila kwenye daftari la wapiga kura,orodha ya wagombea na kwa watu wanaosimamia uchaguzi.Ameuliza je hadi kwa kufikia hatua gani wataweza kusema kuwa hiyo ni hujuma?

Inasemekana kwamba Obasanjo ambaye ni generali mstaafu aliwashinikiza wabunge wa chama tawala cha PDP kumpigira kura Umaro Yar’Adua gavana wa jimbo la Katsina kuwa mgombea wa urais wa chama hicho kwa vitisho vya kuwachunguza kwa kuhusika na hujuma. Obasanjo mwenye umri wa miaka 69 pia alilazimisha kupitishwa kwa kanuni mpya za kumfanya awe mwenyekiti wa chama wa maisha baada ya kun’gatuka urais akiwa anadhibiti masuala ya sera,uwanachama na fedha.

Bunge la Nigeria limemtaka Obasanjo aweke nadhari yake katika sheria hatua inayoonekana kama ni bebeduo kwa dhima yake ya kujaribu kuwafanya baadhi ya wagombea kuwa hawastahiki kuwania uchaguzi huo.Wabunge hao wameorodhesha baadhi ya vifungu vya sheria na katiba na kumtaka Obasanjo avizingatie.

Rais ambaye hatokuwa na mamlaka ya kuungwa mkono na umma mkubwa anaweza kuitumbukiza nchi hiyo kwenye machafuko zaidi.