Kujitowa kwa Mahathir katika chama tawala kunatishia hatamu za Waziri Mkuu Badawi nchini Malaysia.
19 Mei 2008Mahathir Mohamad ambaye alimteuwa binafsi Badawi kuwa mrithi wake hapo mwaka 2003 amesisitiza kwamba hatorudi kwenye chama hicho cha Muungano wa Taifa wa Wamalay UMNO hadi hapo waziri mkuu huyo atakapon'gatuka jambo ambalo limezidisha mashaka ya kisiasa yanayoweza kutibuwa masoko ya fedha.
Akijibu suali la mwandishi wa habari kufuatia wito wa Mahathir wa kumtaka ajiuzulu Abdullah Badawi amejibu kwamba kwanini afanye hivyo na ana kazi ya kufanya na ataendelea na kazi hiyo.Ameongeza kusema kwamba ameshtushwa na kujiuzulu kwa Mahathir.
Haikuweza kufahamika mara moja iwapo Mahathir mwenye umri wa miaka 82 ambaye amekiongoza chama cha UMNO kwa miaka 22 ataunda chama kengine kilichojitenga kupambana na UMNO lakini wachambuzi wa mambo wamesema hatua hiyo ilikuwa imelenga kukitikisa chama hicho ili kuchukuwa hatua dhidi ya Abdullah Badawi na kuenzi urithi walioachiwa na Mahathir.
Naibu waziri mkuu wa zamani Musa Hitam amesema kumekuwako na mazungumzo mengi lakini hakuna vitendo kwa wale wanaompinga Abdullah kwa hiyo Mahathir imebidi achukuwe hatua ya kwanza na kwamba wengi watafuatia.
Ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba inabidi mkutano wa dharura wa UMNO ufanyike kuamuwa juu ya hatima ya waziri mkuu huyo.
Mahathir amezidisha shinikizo kwa Abdullah kujiuzulu baada ya waziri mkuu huyo kukiongoza chama cha UMNO na serikali ya mseto inayoingoza katika kushindwa vibaya wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika hapo mwezi wa Machi.
Kutoka kwake kwenye chama kumekuja siku tatu baada ya Abdullah kumuamuru mwanasheria mkuu wa serikali kumchunguza yeye pamoja na watu wengine watano juu ya uwezekano wa kufanya makosa wakati wa kuwateuwa mahakimu wakati Mahathir akiwa madarakani.
Iwapo wabunge wa chama hicho cha UMNO watajitangaza kuwa huru itamaanisha kwamba hakuna chama kitachokuwa na wingi wa viti bungeni.
Mahathir hapo awali alikaririwa akisema kwamba hatokuwa mwanachama wa UMNO kwa kadri Abdullah atakavyoendelea kuwa rais wa UMNO. Amewaambia waandishi wa habari katika jimbo allikozaliwa la Kedah kwamba amepoteza imani na uwezo wa chama cha UMNO kulinda maslahi ya wananchi wa kabila la Wamalay walio wengi ambao haki zao na upendeleo umekuwa ukichunguzwa na watu wasio wa kabila la Wamalay.
Mahathir ambaye alijiunga na UMNO hapo mwaka 1946 amewataka wanachama wa chama hicho wajiuzulu lakini wasijiunge na upinzani ambao unataka kunyakuwa madaraka kutoka kwa muungano wa vyama tawala vya Barisan National kwa kuwavuta wale wanaokihama chama cha UMNO.
Waziri wa biashara ya ndani Shahir Samad ambaye ni mfuasi wa Abdullah anasema kutoka kwa wingi kwa wanachama kunaweza kuhatarisha kuanguka kwa serikali inayoongozwa na chama hicho cha UNMO.
UNMO ambao ni uti wa mgonggo wa muungano wa vyama 14 tawala wa BN umekuwa ukitawala tokea uhuru wa nchi hiyo kutoka Uingereza hapo mwaka 1957 unashikilia viti 79 kati ya viti 140 vya serikali ya mseto.
Wachambuuzi wa mambo wanasema inaonekana Mahathir amekasirika juu ya madai ya kufanya makosa wakati wa uteuzi wa mahakimu.
Mwenyewe amesema suala hilo ni la mahkama na atakwenda mahkamani kwamba wanaweza kumshtaki ikiwa ana hatia atakwenda gerezani na iwapo hana hatia wasimkamate.