1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Real Madrid, Bayern na Inter zapeta ligi ya mabingwa Ulaya

9 Novemba 2023

Real Madrid, Inter Milan, Real Sociedad, RB Leipzig na Bayern Munich zimekuwa timu za kwanza kufuzu katika raundi ya 16 bora katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya kwa msimu wa mwaka 2023/2024.

https://p.dw.com/p/4YbXK
Fußball Champions League, Bayern München - Galatasaray Istanbul
Wachezaji wa Bayern Munich wakishangilia ushindi katika mchezo wao wa ligi ya mabingwa dhidi ya Galatasaray wa magoli 2 kwa 1.Picha: Bernd Feil/M.i.S./IMAGO

Mabingwa mara 14 wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, Real Madrid wamefuzu raundi ya 16 bora ya michuano hiyo baada ya kuwatwanga Braga ya Ureno kwa magoli matatu kwa bila, dakika ya 27 ya mchezo Brahim Diaz aliweka kambani goli la kwanza kabla ya Vinicius Junior na Rodrygo kufunga bao la pili na tatu mtawalia.

Soma zaidi:Kikosi cha Manchester United kinaendelea kuandamwa na zimwi la kufanya vibaya kuanzia nyumbani hadi mechi za kimataifa 

Mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich wameungana na Real Madrid baada ya kushinda mechi yao ya 17 mfululizo katika hatua ya makundi dhidi ya waturuki Galatasaray 2-1.

Timu zingine ambazo mpaka sasa zimefuzu katika raundi  ya 16 bora ni pamoja na mabingwa watetezi Manchester City ambao walijihakikishia ushindi wa magoli matatu dhidi ya Young Boys, RB Leipzig ya Ujerumani ambayo ipo kundi moja na Man City nayo imejikatia tiketi yake kwenye hatua ya 16 bora.

Soma zaidi: Kane: Bayern itazidi kuimarika msimu unavyosonga

Timu za kundi D za Real Sociedad na Inter Milan pia ayimejikatia tiketi huku Benfica na RB Leipzig wakisubiria tu kutamatisha michezo iliyosalia.

Manchester United'sUnited
Nyota wa Manchester Marcus Rashford alitolewa katika mchezo dhidi ya Copenhagen kwa kadi nyekunduPicha: Dave Thompson/AP/picture alliance

Kwa upande mwingine, Manchester United waliangukia pua huko Denmark baada ya kukubali kichapo cha magoli manne kwa matatu dhidi ya Copenhagen na hivyo watalazimika kusubiri michezo miwili iliyosalia kujua hatma yao katika michuano hii.

Kundi lingine ambalo mpaka sasa hakuna aliyejihakikishia kusonga mbele katika raundi ya 16 bora ni kundi F, Borussia Dortmund ya Ujerumani, AC Milan, PSG na Newcastle United, kila timu kwenye kundi hilo inayo nafasi ya kuweza kusonga mbele.

Mechi za ligi ya mabingwa kwa hatua ya makundi itaendelea tena Novemba 28 na 28 mwaka huu.