1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la Taliban lauteka mji wa 10 Afghanistan

12 Agosti 2021

Wanamgambo wa Taliban wameuteka mji mwengine mkuu wa mkoa Alhamis, huu ukiwa ni mji wa kumi uliotekwa na waasi hao katika kipindi cha mashambulizi ya wiki nzima kote Afghanistan.

https://p.dw.com/p/3ysh6
Afghanistan Ghazni | Taliban Kämpfer
Picha: Gulabuddin Amiri/AP Photo/picture alliance

Haya yanafanyika wakati vikosi vya Marekani na muungano wa kujihami wa NATO vinajiandaa kuondoka kabisa nchini humo baada ya miongo kadhaa ya vita.

Wanamgambo wa Taliban wamepeperusha bendera zao nyeupe zilizo na maandishi yanayoonyesha imani yao ya Kiislamu katika mji wa Ghazni ulioko kilomita 130 kusini magharibi mwa Kabul. Maafisa wawili wa serikali ya mkoa huo wameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa mapigano yameendelea kushuhudiwa katika kambi ya maafisa ujasusi na jeshi nje ya mji huo wa Ghazni.

Mapigano yamekuwa makali sana Kandahar

Afisa mmoja mwandamaizi wa usalama amethibitisha kutekwa kwa mji huo na Taliban. Mji huo uko katika barabara kuu kati ya Kabul na mji wa pili wa Kandahar. Afisa huyo amesema baada ya mapigano makali wanamgambo wa Taliban wamechukua udhibiti wa kila shirika la serikali. Kutekwa kwa mji wa Ghazni ni pigo jengine kwa majeshi ya serikali ya Afghanistan kwani jambo hili litauwekea mji mkuu Kabul shinikizo zaidi.

Afghanistan | Zwischen den Fronten | Taliban erobern Kundus
Wapiganaji wa TalibanPicha: Abdullah Sahil/AP/picture alliance

Mapigano pia yamekuwa makali katika mji wa kusini wa Kandahar. Kulingana na daktari katika hospitali kuu ya mji huo, walipokea miili kadhaa ya majeshi ya serikali na wanamgambo wa Taliban waliojeruhiwa.

Hayo yakiarifiwa huko Doha, Qatar, mjumbe wa Marekani Zalmay Khalilzad amekutana na wanadiplomasia kutoka China, Pakistan na Urusi katika juhudi za kuionya Taliban endapo itaendelea kufanya mashambulizi. Khalilzad anapanga pia kukutana na maafisa wa serikali ya Afghanistan na Taliban. Taliban kupitia msemaji katika afisi yake ya kisiasa Mohammad Naim imesema;

"Tuko hapa Doha na iwapo serikali ya Afghanistan inataka kuendelea kuelekea njia ya kisiasa na kutatua matatizo kupitia mazungumzo tuko tayari na haya yanaweza kuthibitishwa na yale mashambulizi tunayoyafanya na ambayo yanaonekana na dunia nzima. Tunasema tunataka kusuluhisha matatizo kupitia mazungumzo lakini ni uamuzi wao kile wanachopendelea," alisema Naim.

Uturuki inataka kuendesha shughuli uwanja wa ndege wa Kabul

Huku uwezo wa serikali ya Afghanistan kufanya mashambulizi ya angani ukiwa ni mdogo, jeshi la anga la Marekani linaaminika limekuwa likifanya mashambulizi kuyaunga mkono majeshi ya serikali.

Wakati huo huo Uturuki kupitia waziri wake wa ulinzi Hulusi Akar inaamini litakuwa jambo la muhimu iwapo uwanja wa ndege wa Kabul utasalia wazi. Akar ameyasema haya wakati ambapo majadiliano yanaendelea kuhusiana na Uturuki kuendesha shughuli za uwanja huo wa ndege.

Uturuki imejitolea kutuma majeshi katika uwanja huo wa ndege baada ya majeshi ya NATO kuondoka na kuhusiana na hilo imefanya mazungumzo na Marekani kwa wiki kadhaa sasa. Kama malipo kwa huduma hiyo ya Uturukix, rais wa nchi hiyo Rais Reccep Tayyip Erdogan anataka kutimizwe masharti kadhaa ya kifedha na kidiplomasia.