Kura zaendeelea kuhesabiwa uchaguzi wa bunge la Syria
20 Julai 2020Matangazo
Zoezi la kuhesabu kura linaendelea leo Jumatatu nchini Syria baada ya raia nchini humo kupiga kura kuchagua wabunge wapya.
Uchaguzi huo ulifanyika jana Jumapili bila ya kuwepo kwa upinzani wowote kwa chama cha Rais Bashar al-Assad cha Baath.
Mwanachama mmoja katika tume ya uchaguzi nchini humo ameliambia shirika la habari la dpa kuwa zoezi la kuhesabu kura limekamilika kwa asilimia 90.
Uchaguzi huo ni wa tatu kufanyika nchini humo tangu kuzuka kwa uasi wa kupigania demokrasia mwaka 2011.
Uchaguzi huo wa siku moja ulikuwa umeahirishwa mara mbili kuanzia mwezi Aprili kufuatia janga la virusi vya Corona.