1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuuawa Khashoggi, Uturuki yazidi kuishinikiza Saudi Arabia

23 Oktoba 2018

Baraza la Mawaziri la Saudi Arabia limesema litawawajibisha wale wote waliohusika na mauaji ya Jamal Khashoggi bila kujali wao ni kina nani, kikao cha baraza la mawaziri kiliongozwa na mfalme Salman

https://p.dw.com/p/372zL
Saudi Arabien Vision 2030 Präsentation König und Kronprinz
Picha: picture-alliance/abaca/B. Algaloud

Mwandishi huyo alitoweka tarehe 2 mwezi huu baada ya kuingia kwenye ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul. lakini baada ya kukanusha kuwa na habari zozote juu ya mwandishi huyo kwa wiki kadhaa, maafisa wa Saudi Arabia walikiri kwamba aliuliwa ndani ya ubalozi huo na watu waliojiamulia wenyewe kufanya hivyo.

Akiwahutubia  wabunge wa chama chake mapema leo rais wa Uturuki Racep Tayyip Erdogan alisema  kuwa  mauaji hayo yalikuwa ya kudhamiria. Kauli hiyo inakinzana na maelezo yaliyotolewa na Saudi Arabia kwamba Khashoggi aliuawa kwa bahati mbaya.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: Reuters/T. Berkin

Rais Erdogan ameitaka Saudi Arabia iwataje wote waliohusika na mauji hayo bila ya kujali nyadhifa zao.  Rais huyo wa Uturuki pia amesema anataka watu 18 ambao wamekamatwa nchini Saudi Arabia  kuhusiana na mauaji hayo wahukumiwe kwenye mahakama za nchini Uturuki, jambo linaloweza kusababisha utata kwa sababu nchi hiyo ya kifalme imesema kuwa itafanya uchunguzi wake na kwamba itawaadhibu waliohusika. Saudi Arabia imewaita watuhumiwa wa mauaji kuwa ni wahalifu waliojiamuliwa wenyewe, licha ya kuhusishwa kwa maafisa walio karibu na mwanamfalme Mohammmed bin Salman. 

Waziri wa Mambo ya nje wa Saudi Arabia Adel al-Jubeir alipozungumza na shirika la habari la FOX News amelaumu operesheni iliyofanywa na watu makatili ambao amesema walifanya mauaji hayo kwa sababu zao binafsi, watu ambao walikiuka majukumu yao na kisha kujaribu kufunika matendo yao. Jamal Khashoggi aliuawa baada ya kuingia kwenye ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul mnamo tarehe 2 Oktoba, alikwenda ili kuchukua karatasi kwa ajili ya kufunga ndoa na mchumba wake Hatice Cengiz, raia wa Uturuki.

Rais Erdogan amesema nchi yake inataka majibu ya maswali yote ambayo hayajajibiwa na hasa kuhusu nani aliyeamrisha mauaji hayo. Tangu kupatikana habari juu ya kuuawa kwa mwandishi huyo wa gazeti la Washington Post ambaye pia alikuwa mkosoaji mkubwa wa mwana mfalme wa Saudi  Arabia, nchi hiyo ya kiarabu imekuwa chini ya shinikizo kubwa la jumuiya ya  kimataifa.

Mwandishi wa habari aliyeuawa Jamal Khashoggi
Mwandishi wa habari aliyeuawa Jamal Khashoggi Picha: picture-alliance/AA/O. Shagaleh

Wakati huo huo mfalme Salman wa Saudi Arabia na mrithi wa mfalme Mohammed bin Salman wamekutana na familia ya Khashoggi leo Jumanne. Watawala wa Saudi Arabia wamekutana na watoto wa Khashoggi Salah na ndugu yake Sahel kwenye jumba la kifalme mjini Riyadh.

Kwingineko mkurugenzi wa shirika la ujasusi la Marekani CIA Gina Haspel amewasili nchini Uturuki kwa ajili ya kufanya tathmini kuhusu kuuawa kwa Khashoggi. Vilevile viongozi wa Sweden na Denmark wamesema baada ya hotuba ya rais wa Uturuki Rais Recep Tayyip Erdogan mtazamo wao ni kwamba Saudi Arabia inahusika na mauaji ya  Jamal Khashoggi baada ya kupanga njama. Waziri mkuu wa muda wa Sweden Stefan Lofven, amesema inaaminika kuwa kulitokea mambo mabaya na ya kutisha.

Mwandishi:Zainab Aziz/AFPE/AP

Mhariri: Iddi Ssessanga