Kuvuka Bahari ya Mediterrenean ufike hoi au maiti
28 Aprili 2015Je, picha hizi zinaibua hisia zipi miongoni mwa Waafrika wanaoishi hapa Ulaya? .Kila mara nikisikia maneno, 'Mediterrenean' au 'Lampedusa,' ninatetemeka na kuingiwa na huzuni. Hii ni kwa vile ninajua kuwa watu zaidi ninaowaita kuwa wangu, Waafrika wenzangu watatajwa kuhusika katika mkasa wa hivi karibuni au kuzikwa kwenye fuo za mataifa ya Ulaya.
Labda ungenitarajia, mimi Mwafrika, kughadhabishwa na Ulaya. Lakini nina ghadhabu dhidi ya serikali za Afrika kwa kutofanya inavyostahiki.
Ninachoona kuwa si jambo la kawaida ni kwamba hakuna mwengine, katika Ulaya, anayeonekana kuzitarajia serikali za Afrika kulitafutia suala hili suluhu. Wazungu aghalabu husema wanahitaji kutafuta suluhu, wanahitaji kuboresha hali katika sehemu wanakotokea wahamiaji hawa. Lakini hawaonekani kutumainia au kutarajia serikali za Afrika kusaidia kutafuta suluhu hiyo. Waafrika hawahitaji kusikitikiwa na Wazungu, wanachohitaji ni uwajibikaji.
Ulaya inafaidi kutokana na hali hii ya wafanyakazi kutoka Afrika wanaolipwa ujira mdogo, kweli! Wavuvi wanajipatia vya bwerere katika sehemu maarufu za maji karibu na Afrika. Kakao, matunda, mboga na maua yote yanakuzwa katika bara letu kisha kusafirishwa kwa meli hadi Ulaya na maeneo mengine duniani. Lakini hakuna anayetaka Waafrika kusafiri pamoja na bidhaa zinazosafirishwa kutoka bara letu.
Tangu Ulaya ilipoanza kuangazia suala hilo, imeitisha kikao kimoja tu kuhusu Afrika mjini Kigali. Ninatilia shaka iwapo pendekezo lolote miongoni mwa yaliyotokana na kikao hicho, litatekelezwa.
Ninaamini kuwa tatizo hili linafaa kuwa tatizo la Afrika, ndipo litakaposuluhishwa. Ninafedheheka nikiwa Mwafrika na kufedheheshwa na serikali za bara langu. Changamoto kuu inayotukabili ni kubadili mtazamo wa Waafrika kuhusu Ulaya. Si paradilo kwa wengi wao, ni jahanamu.
Nimekutana na Waafrika walioko Ulaya, wanaolipwa dola 3 kwa siku au chini ya hapo. Kulala ni tabu. Wanauza bidhaa haramu na kutumiwa visivyo au kulazimika kufanya kazi katika maeneo hatari au kushiriki ukahaba. Maisha yao wakiwa Ulaya, huwa mabaya kuzidi ya waliowaacha nyumbani.
Ulaya inasalia kuwa eneo lenye madhara kwa Waafrika wengi. Nilipoishi Italia, nilipokuwa chuoni, aghalabu wanaume walinisogelea na kuniuliza, niligharimu fedha ngapi kwa usiku mmoja. Kile ninachotaka kuwaambia Waafrika wenzangu ni kuwa, ondoeni dhana kwamba Ulaya itatatua matatizo yenu. Upo uwezekano kwamba utaishi katika mitaa duni huku pia.
Ni wakati wa kuzinduka na kumwezesha kila mmoja ajikimu katika taifa lake, badala ya kuwa na matarajio makubwa kuhusu mambo yasiyokuwapo.
Mwadishi: Asumpta Lattus
Tafsiri: Geoffrey Mung'ou
Mhariri: Mohammed Khelef