1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuwajibka kwa pamoja na suala la watu waliopotezewa makaazi

Mohamed Dahman23 Mei 2016

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki wataka kuwepo kwa kanuni madhubuti za kibinaadamu wakati viongozi wa dunia wakikutana kujadili mfumo wa misaada ya kibinaadamu uliosambaratika.

https://p.dw.com/p/1ItEH
Mkutano wa kujadili misaada ya kibinadamu Istanbul
Picha: picture-alliance/AA/A.H. Yaman

"Tuko hapa kujenga mustakbali mpya. Leo tunatangaza ubinaadamu mmoja wenye majukumu sawa ya pamoja. Waheshimiwa mabibi na mabwana tuazimie hapa na hivi sasa sio tu kuwabakisha watu hai bali kuwapa watu fursa ya kuwa na maisha yenye utu."

Hayo yametamkwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon Jumatatu (23.05.2016) wakati akifunguwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa mjini Istanbul ambao unatajwa kuwa wa kwanza wa aina yake kubuni hatua muafaka zaidi za kukabiliana na kile kinachoitwa kuwa mzozo mbaya kabisa wa kibinaadamu kuwahi kushuhudiwa tokea kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kuandaa michango zaidi pamoja na kufikia makubaliano ya kuwahudumia vizuri zaidi watu waliopotezewa makaazi yao.

Ban amezitaka serikali, kampuni za biashara na mashirika ya misaada kupunguza kwa nusu idadi ya watu waliopotezewa makaazi ifikapo mwaka 2030. Jambo hilo yumkini likawa gumu kulifanikisha shirika la madakatari wasiokuwa na mipaka lilijitowa katika mkutano huo mapema mwezi huu kwa kusema kwamba limepoteza matumaini kwamba washiriki wataweza kulishughulikia suala la udhaifu katika kukabiliana na masuala ya dharura.

Wakosoaji wanasema mfumo wa misaada duniani unahitaji kugharimiwa kwa kiwango kikubwa zaidi ili kukabiliana na kuzagaa kwa vita vya kimaeneo ambavyo vimechochea kuongezeka kwa idadi ya watu waliopotezewa makaazi yao na kusambaratika kwa mataifa pamoja na kupunguza ukosefu wa ufanisi na kuwepo rushwa mambo ambayo humeza kima kikubwa cha fedha za misaada ya kibinaadamu kabla ya hata kuwafikia walengwa.

Uwajibikaji wa pamoja

Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki akizungumza katika mkutano huo amesema nchi yake yenye kuhifadhi takriban wakimbizi milioni tatu kutoka Syria inataraji mataifa yatashirikiana katika kutimiza majukumu ya kukabiliana na janga la wakimbizi na wahamiaji.

Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.
Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.Picha: Reuters/M. Sezer

Erdogan amesema: "Tukiwa kama viongozi na watu wenye kuwajibika wa jamii ya kimataifa tunaweza tu kufanikiwa iwapo tutashirikiana kufanikisha kanuni na malengo ya pamoja."

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akizungumza katika mkutano huo ametowa wito wa kuwepo kwa maafikiano mapya duniani kuhusu kanuni za ubinadamu na kuna haja ya kuboresha utowaji wa misaada ya kibinaadamu.

Merkel amesema Ujerumani inaunga mkono pendekezo la kuongeza kima cha michango ya kukabiliana na hali ya dharura kufikia dola bilioni moja ambapo kwa upande wa Ujerumani itatumia fedha zaidi kwa misaada ya kibinaadamu.

Merkel akutana na Erdogan

Mkutano huo wa kilele unakusudia kukusanya michango na kuwafanya viongozi wa dunia wakubaliane juu ya masuala kuanzia na namna ya kuwashughulikia raia waliopotezewa makaazi hadi kujizatiti upya kwa sheria ya kimataifa ya ubinaadamu.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki.Picha: Reuters/K. Ozer/Presidential Palace

Kwa upande mwengine kandoni mwa mkutano huo, Kansela Merkel na Rais Erdogan wamekubaliana kuwa na mikutano kujadili masuala nyeti na vipau mbele vya Uturuki katika vita dhidi ya ugaidi. Hayo yanafuatia kauli ya Kansela Merkel wiki iliopita, kwamba uamuzi wa kuwaondolea kinga ya kutoshtakiwa robo ya wabunge wengi wao wakiwa Wakurdi kuwa tukio linalotia wasiwasi.

Erdogan anawalaumu wabunge wa Kikurdi kuwa wanakiunga mkono chama kilichopigwa marufuku cha PKK na ambacho kinapigana na jeshi la Uturuki.

Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman