Kwa nini nchi za Afrika zinataka kujitoa ICC auliza Bensouda
23 Novemba 2016Mwendesha mashtaka huyo mkuu wa mahakama ya ICC, alitoa maelezo hayo wakati baraza kuu linaloisimamia ICC lilipokutana kujadili swala la nchi za Afrika kutaka kujiondoa kutoka kwenye mahakama hiyo ya ICC. Afrika Kusini, Burundi na Gambia zimetangaza nia ya kujiondoa kutoka kwenye mkataba wa Roma. Nchi 124 ni wanachama wa mkataba huo.
Bensouda katika mahojiano yake na shirika la habari la AFP, amesema badala ya kujitoa kwenye mkataba wa Roma, bara la Afrika linapaswa kushirikiana na ofisi yake ili kuimaliza kabisa tabia ya kudharau sheria, aliongeza kusema kwamba mahakama za kikanda pamoja na za kawaida katika bara hilo zinapaswa kufanya kazi pamoja na ofisi yake katika kuwawajibisha wale wanaosababisha madhila ya kikatili kwa kuwafikisha mbele ya sheria kwa ajili ya kuwatafutia haki wahanga wa ukatili.
Naye wakili anayetetea haki za binadamu Reed Brody ambaye kwa miaka mingi anajaribu kumfikisha katika mahakama ya ICC aliyekuwa rais wa Chad dikteta Hissene Habre amesema anafikiria kwamba kila mmoja angefurahi iwapo kesi kama hizo zingekuwa zinasikiliziwa huko huko barani Afrika. Brody ametolea mfano mahakama ya Senegal ilipomuhukumu kiongozi huyo wa zamani. Habre alipatikana na hatia ya ukatili dhidi ya binadamu, mateso na unyanyasaji wa kimapenzi, makosa ambayo aliyafanya kati ya mwaka 1982 na mwaka 1990 alipokuwa kiongozi wa nchi yake. Habre alihukumiwa kifungo cha maisha.
Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa amesema kwamba ana imani bajeti waliyoipendekeza ya dola milioni 147 kwa mwaka 2017 itaungwa mkono na nchi zote wanachama. Amesema lengo lake ni kupanua jitihada za uchunguzi kazi ambayo inafanywa na ofisi yake. Wakati huo huo Bensouda amefahamisha juu ya nia yake ya kuanzisha uchunguzi unaohusiana na Afghanistan ambapo huenda majeshi ya Marekani na maafisa wa CIA, wapiganaji wa kundi la Taliban na majeshi ya Afghanistan watawajibishwa. Alipoulizwa iwapo ushindi wa rais mteule wa Marekani Donald Trump unaweza kutatiza juhudi zake hizo alijibu kuwa wanazitolea mwito serikali zote na wale wote ambao wanafikiria kuwa ni muhimu kushirikiana nao. Amesema kwamba ofisi yake itaendelea kufanya kazi kwa bidii bila kujali ni serikali gani iko madarakani.
Mwandishi: Zainab AZIZ/APE
Mhariri:Josephat Charo