1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kweli Israel ina nia ya kuikabidhi Palestina maeneo yake

Saumu9 Machi 2005

Kama vile kigeugeu Israel imekataa kufikia uamuzi wa kuondoka maeneo ya wapalestina ya Jericho na Tulkarem

https://p.dw.com/p/CEGD

Habari tulizozipata hivi punde ni kwamba mazungumzo kati ya Isarel na Palestina ya kuondoka kwa majeshi ya Israel katika maeneo ya wapalestina yamesambaratika bila kupatikana jawabu.

Haj ismail Jabir mkuu wa majeshi wa Palestina katika magharibi mwa gaza amesema mkutano kati maafisa wa usalama wa Palestina na maasfisa wa Israel umeshindwa kulifikia lengo la kuondoka kwa majeshi ya Israel katika eneo la Jericho,baada ya kutofautiana juu ya kuondolewa kwa vituo vya kijeshi huko Jericho.

Kabla ya hapo ilidhihirika kana kwamba kulikuwepo na njia ya kuelekea kupatikana salama huko Palestina ,Hapo jana waziri anayehusika na masuala ya Usalama nchini Israel alitangaza kwamba nchi yake huenda ikawarejeshea wapalestina miji yao iliyoko magharibi mwa Gaza ya Jericho na Tulkarem hivi karibuni, huku kiongozi wa Palestina naye upande wake akisema vikundi vya wanamgambo wakipalestina vitakutana mjini cairo Marchi 15 katika kile alichokiita mwito wa kuelekea Umoja wa kitaifa.

Mkutano huo wa vikundi mbalimbali kimsingi ulipangiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi Marchi, lakini hilo halikuwezekana kufuatia shambulio la hivi majuzi mjini Tel Aviv lilofanywa na mwanamgambo wa kundi la Islamic Jihad na kuwauwa waisreal watano.

Na sasa,kwa mujibu wa Jibril Rajub mshauri wa masuala ya kiusalama nchini Palestina,makundi yote ya wapiganaji nchini humo yamethibitisha kwamba yapo tayari kuacha mashambulio dhidi ya Israel na katika maeneo yanayokaliwa na waisrael.

Akiyataja maendeleo hayo kuwa mabadiliko ya kihistoria,Amesema pia kumefikiwa uamuzi ambapo makundi yote yameahidi kusitisha mashambulio ili kutoa nafasi kwa serikali ya Palestina kuafikiana juu ya makubalianoya kuondoka Gaza.

Lakini huku hayo yakiarifiwa Kundi la hamas limetoa sauti tofauti na Jibril, likipinga vikali kufanyika mashauriano yoyote ya kukomesha mashambulio dhidi ya Israel , likisema kuwa ilimradi kunakuwepo na sera za udanganyifu na mazowea ya kuhairisha hatua ya kuondoka gaza upande wa Isarel,basi hakuna chochote kitakachowashawishi kufikia makubaliano ya amani.

Kwa mujibu wa msemaji wa kundi lenye siasa kali la Hamas, Sami Abu Zuhri matamshi ya Jibril sio ya kweli na hana haki ya kuzungumza kwa niaba ya makundi yote.

Lakini hata na hivyo Zuhri anasema mkutano wa cairo watahudhuria lakini haijamaanisha wamekubaliana na mapendekezo yoyote yaliyotolewa bali wanakwenda kusikiliza mapendekezo yatakayotolewa kwenye mkutano huo na baadae wataamua juu ya msimamo watakaochukua.

Amesisitiza pia kundi la Hamas katu halitakoma kuipiga vita Israel iwapo haitaweza kuheshimu masharti ya Palestina yakutaka kuachiwa huru kwa wafungwa wake walioko kwenye jela za Israel.

Hata hivyo kundi la hamas limetangaza kwamba lipo tayari kushirikiana na chama cha PLO na kujitosa kwenye uchaguzi wa wabunge ifikapo mwezi july.