Labadia aachia ngazi VFB Stuttgart
26 Agosti 2013Hewa kwa kocha wa VFB Stuttgart ilizidi kuwa nyepesi na kuumiza kichwa kama mtu anayepanda mlima mrefu baada ya timu hiyo kigogo cha soka nchini Ujerumani kupokea kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya FC Augsburg jana Jumapili.
Mashabiki waliimba , Bruno aondolewe, tangu pale timu hiyo ilipopokea kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Bayer Leverkusen na jana kukubali kipigo cha bao 2-1 dhidi ya Augsburg. Kocha wa FC Augsburg Markus Weinzierl wakati huo huo amesema amefurahishwa na ushindi huo.
"Kwa hakika tumefurahi sana, hilo ni wazi. Nawapongeza pia wachezaji wangu kwa kupata ushindi katika mchezo huu. Ni faraja kubwa kabisa kwetu. Nafikiri, tulistahili pia kushinda, kwasababu katika kipindi cha kwanza tulikuwa tuko mbele kwa mabao 2-0, na tulikuwa tunafanya vizuri, na katika wakati sahihi tumeweza kupata mabao. Tulistahi pia kuongoza katika mchezo huo".
VFB Stuttgart ilisema inatosha na ahsante sana kwa kocha Bruno Labadia na kuachana na huduma zake kuanzia leo Jumatatu(26.08.2013).
Labadia ambaye alijiunga na Stuttgart mwishoni mwa mwaka 2010 , anakuwa kocha wa kwanza msimu huu kufutwa kazi baada ya michezo mitatu ya ligi.
Mshambuliaji huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 47, ambaye pia aliwahi kuifunza Bayer Leverkusen na Hamburg SV, aliiokoa Stuttgart dhidi ya kushuka daraja mwaka 2011 na kuiongoza hadi kuingia katika ligi ya Ulaya msimu uliofuata.
Alipata mafanikio makubwa katika klabu hiyo baada ya kufikia fainali ya kombe la shirikisho DFB Pokal msimu uliopita, ambapo ilishindwa tu kuhimili vishindo vya Bayern Munich ambayo ilikamilisha ushindi wa vikombe vitatu katika msimu mmoja.
Borussia yapeta
Mwanzoni mwa mchezo wa tatu wa Bundesliga Borussia Dortmund iliendeleza ushindi wake msimu huu dhidi ya Werder Bremen kwa bao 1-0 nyumbani , wakati Bayern Munich ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Nürnberg.
Bayer Leverkusen haikuachwa nyuma katika kundi hilo la timu tatu zilizoanza vizuri msimu huu, baada ya kupata tena ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Borussia Moenchengladbach. Dortmund inaongoza msimamo wa ligi ikifuatiwa na Bayer Leverkusen na Bayern Munich.
Wakati huo huo mabingwa wa Ulaya Bayern Munich watakuwa wageni wa Freiburg kesho Jumanne , wakiwania kunyakua ushindi wao wa nne mfululizo katika Bundesliga kabla ya kusafiri hadi mjini Prague ambapo itapambana na Chelsea katika taji la Ulaya la Super Cup.
Hata hivyo Bayern ilipata pigo mwishoni mwa juma baada ya kupata taarifa kuwa mchezaji wake mpya Thiago Alcantara anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa wiki saba kutokana na majeraha aliyoyapata katika mchezo dhidi ya Nürnberg na anatarajiwa kufanyiwa operesheni leo Jumatatu.
Manchester City kurudi sokoni
Mabao mawili kutoka kwa Fraizer Campbell yaliwapa ushindi wa kushangaza wa mabao 3-2 Cardiff City dhidi ya Manchester City jana Jumapili wakati timu hiyo inayoshiriki kwa mara ya kwanza katika Premier League ikisherehekea ushindi wake wa kukumbukwa katika ligi hiyo nyumbani katika muda wa miaka 51.
Manchester City huenda wakaingia sokoni tena kusaka wachezaji wa ulinzi baada ya kipigo hicho cha kushitua, kilichoweka wazi matatizo ya ulinzi.
Katika michezo mingine jana Tottenham Hot Spurs ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Swansea City. Wakati siku ya Jumamosi Lukas Podolski ambaye kuwa uvumi kuwa huenda akarejea katika Bundesliga katika timu ya Schalke 04 kabla ya mwishoni mwa mwezi huu , alipachika mabao mawili katika ushindi wa timu yake ya Arsenal London wa mabao 3-1 dhidi ya Fulham.
Manchester United inamiadi leo usiku na Chelsea katika mchezo ambao unazikutanisha timu mbili ambazo zinaonekana zitakabana koo katika kuwania ubingwa wa Premier League msimu huu.
Wakati huo huo vita ya maneno imeanza kati ya Chelsea na Manchester United, sio kuhusu mchezo wao huo jioni ya leo lakini ni kuhusu mshambuliaji Wayne Rooney.
Kocha wa Chelsea Jose Mourinho amesema kuwa kocha wa Manchester United David Moyes anapaswa kubeba lawama kutokana na nia ya Wayne Rooney kutaka kuihama timu hiyo ya Old Trafford. Chelsea imetoa ombi la kumtaka Rooney kujiunga na timu hiyo mara mbili na haijaondoa uwezekano wa kufanya hivyo tena.
Rooney anasemekana kuwa amekasirishwa na matamshi ya Moyes kuwa atakuwa chaguo la pili iwapo Robin van Persie atakuwa majeruhi. Alipoulizwa Mourinho iwapo anatarajia hasira za mashabiki wa Manchester jioni ya leo alijibu, na hapa namnukuu ; hawastahili kupambana na mimi, iwapo nitasema Ramires atakuwa chaguo la pili wakati Frank Lampard atakuwa amechoka ama majeruhi, na iwapo mtu atakuja hapa na kumhitaji Ramires hakuna mtu atakayekasirika. Mwisho wa kumnukuu.
Barca yanusurika
FC Barcelona iliweza kunusurika mara kadha katika kipindi cha pili dhidi ya mashambulio ya Malaga na kufanikiwa kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 jana Jumapili na kuendeleza mwanzo mzuri katika msimu huu. Wakati huo huo Atletico Madrid ambayo iko nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ya Uhispania La Liga ilipata karamu ya magoli dhidi ya Rayo Valecano kwa kuigaragaza kwa mabao 5-0 jana Jumapili.
Nchini Italia Carlos Tevez alipata bao lake la kwanza katika ligi ya nchi hiyo Serie A baada ya mabingwa watetezi Juventus Turin ilipopata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Sampdoria . Napoli iliishinda Bologna kwa mabao 3-0.
Nchini Ufaransa Paris St Germain iliishinda Nantes kwa mabao 2-1 jana Jumapili, wakati Olympique Marseille ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Valenciennes siku ya Jumamosi.
Tanzia
Mlinda mlango Gilmar wa timu ya taifa ya Brazil ambayo ilipata ubingwa wa dunia mwaka 1958 na 1962 amefariki dunia mjini Sao Paolo akiwa na umri wa miaka 83. Mlinda mlango huyo wa zamani wa Santos FC na Corinthians amepata mshtuko wa moyo wiki iliyopita na hakuweza kuhimili hali hiyo hadi kufariki. Amekuwa katika hali mbaya ya afya kwa miaka kadha baada ya kupata kiharusi.
Kocha wa Tottenham Hotspurs Andre Villas-Boas amesisitiza kuwa uhamisho wa Gareth Bale kutoka timu hiyo kwenda Real Madrid haujakamilika, lakini anatarajia majadiliano yataendelea katika saa 48 zijazo.
Bale alikuwa mjini Madrid wakati timu yake ilipopata ushindi dhidi ya Swasea City na kupata ushindi wa pili mfululizo katika Premier League.
Mbio za magari:
Sebastian Vettel amepata tena ushindi na dereva huyo wa Red Bull sasa ana points 46 mbele ya Fernando Alonso wa magari ya Ferrari katika msimamo wa Formula one kabla ya mbio zitakazofanyika huko barani Asia ambako Mjerumani huyo ametamba katika miaka iliyopita.
Katika mbio 14 zilizofanyika katika bara la Asia katika misimu mitatu iliyopita, Vettel ameshinda mara tisa.
Golf.
Wachezaji mahiri kutoka bara la ulaya na Asia watakabiliana kila baada ya miaka miwili katika kinyang'anyiro kipya cha mchezo wa golf nchini Malaysia katika mtindo wa kombe la Ryder unaokutanisha wachezaji wa golf wa Ulaya na Marekani.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / ape / dpae / rtre
Mhariri: Yusuf Saumu