1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LAGOS : Mbabe wa vita Nigeria yumkini kukabiliwa na hukumu ya kifo

24 Septemba 2005
https://p.dw.com/p/CEYG

Kiongozi wa wanamgambo wa Nigeria Alhaji Mujahidi Dokubo Asari anashikiliwa chini ya ulinzi mkali katika nyumba ya binafsi mjini Abuja na yumkini akakabiliwa na hukumu ya kifo iwapo atakutikana na hatia ya uhaini.

Wakili wake Oche Okwukwu ambaye mwenyewe binafsi alitiwa mbaroni wakati alipokwenda katika mji mkuu huo wa Nigeria kumtetea Asari amesema hapo jana kwamba nia iliyotangazwa na serikali ni kumshtaki mwanamgambo huyo wa kikabila kwa uhaini jambo ambalo litaamanisha mojawapo ya mambo mawili.

Okwukwu ameliambia shirika la habari la AFP baada ya kuachiliwa kwa dhamana kwamba iwapo Asari atapatikana moja kwa moja na hatia ya uhaini hukumu yake itakuwa ni kifo na wakati akionekana na hatia ya kosa la uhaini hukumu yake itakuwa kifungo cha maisha gerezani.

Asari alikamatwa hapo Jumanne baada ya kukaririwa katika mahojiano na gazeti akitishia kuchukuwa silaha kuhakikisha kuvunjika kwa Nigeria.

Kukamatwa kwake kumechochea hasira miongoni mwa wafuasi wake waliomo katika kundi lililopigwa marufuku la Valantia la Watu wa Niger Delta ambalo uongozi wake uliobakia umeapa kuteketeza miundo mbinu ya mafuta ya jimbo la Niger Delta venginevyo anaachiliwa.