LAGOS: Rais Obasanjo atia makali ufagio wa rushwa Nigeria.
6 Aprili 2005Spika wa Bunge la Nigeria Adolphus Wabara aliyechukuliwa kuwa na uwezo mkubwa wa kisiasa amejiuzulu wadhfa wake kufuatia tuhuma za rushwa.
Bwana Wabara amehusishwa na kashfa ya kupokea zaidi ya Euro laki tatu ili kuupitisha mswada wa bajeti ya elimu.
Amesema kuwa amejiuzulu wadhfa wake ili ajitetee na tuhuma hiyo dhidi yake.
Katika kutilia mkazo vita dhidi ya rushwa nchini Nigeria rais Olusegun Obasanjo pia amemtimua kutoka mamlakani waziri wake wa ujenzi na nyumba kwa tuhuma za kuwauzia maafisa wakuu nyumba za serikali kisiri.
Kamishna wa zamani wa polisi nchini Nigeria tayari nae amefikishwa mahakami kwa kosa la kutumia vibaya kiasi cha Euro millioni 78 fedha za serikali.
Shirika la Transparency International lenye makao yake mjini Berlin katika ripoti yake limeitaja Nigeria kuwa nchi ya tatu duniani inayokabiliwa na visa vilivyo kithiri vya rushwa.