Laschet kugombea nafasi ya ukansela
20 Aprili 2021Laschet atawania kinyang'anyiro hicho baada ya mpinzani wake mkuu Markus Soeder, waziri mkuu wa jimbo la Bavaria na kiongozi wa chama ndugu cha CSU kukubali kushindwa.
Soeder ameuchukua uamuzi huo baada ya chama cha CDU kumuunga mkono Laschet, mwenye umri wa miaka 60 katika mkutano uliofanyika usiku wa kuamkia leo. Akizungumza mjini Munich, Soeder amesema Laschet ndiyo atakuwa mgombea wa ukansela wa muungano huo na kwamba amempigia simu kumpongeza.
"Tutamuunga mkono bila kinyongo, kwa nguvu zetu zote. Naweza kusema hayo mimi mwenyewe, lakini naamini pia sisi kama CSU, hilo ndilo tutakalofanya. Jambo muhimu kwa sasa ni kusimama pamoja na kuondoa tofauti," Soeder.
Laschet amemshukuru Soeder baada ya kushinda nafasi hiyo katika mchuano wa ndani. Akizungumza na waandishi habari Laschet amesema kupitia mazungumzo wamefanikiwa kuona maisha ya demokrasia.
Laschet sasa anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuwavutia wapiga kura ambao hawajaridhishwa na jinsi serikali ilivyolishughulikia janga la COVID-19.
Laschet ambaye hana umaarufu wa umma kama ilivyo kwa Soeder, baada ya utafiti wa maoni wa hivi karibuni uliofanywa na gazeti la kila siku la Handelsblatt kuonesha kuwa ni maarufu, huku asilimia 12 ya Wajerumani wakisema wanahisi atakuwa mgombea mzuri wa ukansela.
Aidha, Katibu Mkuu wa chama cha CDU, Paul Ziemiak amesema Laschet ni mgombea sahihi wa ukansela nchini Ujerumani.
Akizungumza pembezoni mwa Soeder mjini Munich, Katibu Mkuu wa CSU Markus Blume amesema chama chake kinayaheshimu matokeo hayo. Blume amesema Soeder alitambuliwa kama mgombea aliyeko mioyoni mwao, lakini demokrasia ndani ya chama imeamua.
Kansela Angela Merkel amempongeza Laschet baada ya kuchaguliwa kuwa mgombea wa ukansela wa shirikisho. Kupitia msemaji wake, Steffen Seibert, katika ukurasa wa Twitter, Merkel amesema yuko tayari kufanya kazi pamoja na anatarajia ushirikiano mzuri katika miezi inayokuja.
Kansela Merkel ambaye amekiongoza chama hicho cha kihafidhina na aliyeiongoza Ujerumani kwa miaka 16 atajiuzulu wadhifa wake baada ya uchaguzi wa Septemba 26.
Siku ya Jumatatu chama cha watetezi wa mazingira cha Kijani kilimchagua Annalena Baerbock kuwa mgombea wake wa ukansela. Chama cha SPD kilimchagua mgombea wake wa ukansela, Olaf Scholz miezi michache iliyopita.
(DPA, AP, AFP, Reuters)