1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais mpya Lebanon: Matumaini ya utulivu Mashariki ya Kati

13 Januari 2025

Joseph Aoun ana uungwaji mkono mkubwa, ikiwemo kutoka Hezbollah na Israel. Hili linaweza kuwa muhimu katika kuimarisha usitishaji vita baina ya Israel na Hezbollah pamoja na kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa uchumi.

https://p.dw.com/p/4p3zG
Lebanon Beirut 2025 | Joseph Aoun atoa hotuba ya kwanza kama rais mpya aliyechaguliwa bungeni
Rais wa Lebanon Joseph Aoun anaonekana kama mdhamini wa uthabiti wa nchi hiyo iliyokumbwa na vitaPicha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Kuchaguliwa kwa rais mpya wa Lebanon, Joseph Aoun, Alhamisi (Januari 9), kulihitimisha kipindi cha miaka miwili cha ombwe la kisiasa chini ya serikali iliyokuwa ya mpito. 

"Aoun alionekana kama mgombea anayeweza kuleta utulivu baada ya kipindi kirefu cha misukosuko nchini Lebanon," alisema Kelly Petillo, mtafiti wa Mashariki ya Kati katika Baraza la Uhusiano wa Kigeni la Ulaya (ECFR), katika mazungumzo na DW. 

Hata hivyo, alisema uchaguzi huo "haukuwa rahisi." 

"Katika raundi ya kwanza ya kupiga kura, Aoun hakuweza kupata kura 86 zilizohitajika ili kushinda urais," Petillo alieleza. 

Aliongeza kuwa tawi la kisiasa la Hezbollah pamoja na mshirika wake wa bunge, Vuguvugu la Amal, walijizuia kupiga kura. 

Tawi la kijeshi la Hezbollah linachukuliwa kama kundi la kigaidi na nchi kadhaa, ikiwemo Marekani na Umoja wa Ulaya. Kwa upande mwingine, tawi lake la kisiasa linawakilishwa bungeni na linashughulika sana na masuala ya ustawi wa jamii. 

Soma pia:Israel yasitisha vita Lebanon na kuendelea kuishambulia Gaza 

"Kabla ya raundi ya pili ya upigaji kura kufanyika, Hezbollah na mavuguvugu yanayohusiana na jamii ya Waislamu wa Shia wa Lebanon walipewa uhakika kwamba kumpigia kura Aoun ndilo lilikuwa suluhisho pekee la kuleta msaada muhimu wa kikanda na Kimagharibi kwa nchi ambayo uchumi wake uko taabani," Petillo alisema. 

Rais wa Lebanon Joseph Aoun
Aoun sasa analo jukumu la kusimamia uendelezaji wa mpango wa kusitisha vita kati ya Israel na Hezbollah.Picha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Aliongeza kuwa vyama vya Kishia pia vilihakikishiwa uwakilishi wa kutosha katika serikali mpya ya Lebanon. 

"Kwa msingi huo, kulikuwa na raundi ya pili ambapo hatimaye Aoun alifanikiwa kupata kura 99 kati ya viti 128 vya bunge," Petillo alisema. 

Wakati huo huo, viongozi wa serikali kutoka Iran, Israel, Marekani, Ufaransa, na wengine wengi walimpongeza Joseph Aoun, ambaye hana uhusiano wa kifamilia na rais wa zamani Michel Aoun. 

"Leo, awamu mpya katika historia ya Lebanon inaanza," alisema Jenerali Aoun, aliyekuwa mkuu wa jeshi la Lebanon kabla ya kuchaguliwa, wakati akihutubia wabunge jijini Beirut baada ya kula kiapo. 

Joseph Aoun mwenye umri wa miaka 61, ambaye aliteuliwa kuwa mkuu wa jeshi mnamo Machi 2017, aliweka majeshi ya Lebanon kando na mgogoro kati ya Israel na Hezbollah ambao uliongezeka baada ya miezi 12 ya mapigano madogo na kuwa vita vya wiki nane ambapo Hezbollah ilidhoofishwa sana na zaidi ya watu 3,000 waliuawa. 

Uchaguzi wa rais wa Lebanon ulitangazwa mwishoni mwa Novemba, siku moja baada ya kuanza kwa usitishaji mapigano wa siku 60 kati ya Hezbollah na Israel. 

Kura hiyo ya Alhamisi ilifanyika takriban wiki mbili kabla ya kumalizika rasmi kwa muda wa usitishaji huo wa mapigano. 

Jukumu la Joseph Aoun sasa ni kuimarisha usitishaji huo wa mapigano. 

Kama sehemu ya makubaliano hayo, jeshi la Lebanon litalazimika kupeleka wanajeshi pamoja na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kusini mwa Lebanon. 

Israel, kwa upande wake, italazimika kuondoa wanajeshi wake kutoka ardhi ya Lebanon, huku Hezbollah ikitakiwa kupeleka vikosi vyake kilomita 40 kaskazini mwa Mto Litani wa Lebanon. 

Lebanon Beirut 2025 | Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Antonio Tajani katika mkutano na waandishi wa habari mjini Damascus
Rais mpya wa Lebanon akikutana na waziri wa mambo ya nje wa Italia, Antonio Tajani mjini Beirut, Januari 10, 2025.Picha: Lebanese Presidency/AFP

"Aoun atahakikisha kuwa jeshi la Lebanon litazingatia makubaliano ya usitishaji mapigano kwa msaada wa kifedha na kisiasa kutoka nchi za Magharibi na zile zinazoiunga mkono Israel," alisema Lorenzo Trombetta, mchambuzi wa Mashariki ya Kati na mshauri wa mashirika ya Umoja wa Mataifa ambaye amekuwa akiishi Beirut kwa miaka 20 iliyopita, alipokuwa akizungumza na DW. 

Soma pia: Israel na Lebanon zakubali masharti ya kusitisha vita

"Pia, Hezbollah imelazimika kutambua hali mpya iliyopo baada ya kushindwa wakati wa msimu huu wa vuli na kumpoteza kiongozi wake, Hassan Nasrallah," aliongeza. 

Maoni haya yanashabihiana na yale ya Kelly Petillo. "Kumekuwa na mabadiliko makubwa kuhusu ushawishi wa Hezbollah na Iran kwani walipata pigo kubwa kutokana na vita vya Gaza na athari zake kwa Lebanon," alisema, akiongeza kuwa kuanguka kwa utawala wa Assad wa Syria unaoungwa mkono na Iran pia kumeidhoofisha Hezbollah na Iran. 

Hata hivyo, inasubiriwa kuonekana kama Israel na Hezbollah, ambao wamekuwa wakituhumiana kukiuka usitishaji wa mapigano na kutishia kuuvunja ikiwa upande wowote utakiuka masharti, watatii makubaliano hayo. 

Tahadhari kuhusu mdororo wa kiuchumi Lebanon

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa mpito wa Lebanon, Najib Mikati, alisema Ijumaa kuwa serikali iko mbioni kuanza mchakato wa kuondoa silaha kusini mwa Lebanon. 

"Tuko katika awamu mpya," Mikati alisema, akieleza kuwa "katika awamu hii mpya, tutaanza na kusini mwa Lebanon na kusini mwa Litani haswa ili kuondoa silaha ili serikali iweze kuwapo katika maeneo yote ya Lebanon." 

Kuimarisha uchumi 

Hii inatarajiwa kuwa mojawapo ya kauli za mwisho za Mikati kama waziri mkuu wa mpito. Mojawapo ya kazi za kwanza za Rais Joseph Aoun itakuwa kumteua waziri mkuu mpya haraka iwezekanavyo. 

Kulingana na mfumo uliowekwa wa kugawana madaraka nchini humo, waziri mkuu anatakiwa kuwa Mwislamu wa madhehebu ya Sunni, rais anatakiwa kuwa Mkristo wa dhehebu la Maronite, na spika wa bunge awe Mwislamu wa madhehebu ya Shia. 

Mojawapo ya majukumu makubwa ya waziri mkuu mpya itakuwa kusimamia mfululizo wa mageuzi ya kiuchumi yanayohitajika ili kukidhi mahitaji ya wakopeshaji wa kimataifa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). 

Uharibifu wa Lebanon huko Nabatieh baada ya mashambulio ya Israeli
Uchumi wa Lebanon ni dhaifu sana kuweza kufadhili ujenzi wa sehemu za Beirut na Kusini mwa nchi na inategemea msaada wa kimataifa.Picha: Jose Colon/Anadolu/picture alliance

Bila msaada wa kimataifa, nchi hiyo inayokabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi itapata shida kukabiliana na mfumuko wa bei uliopanda kwa kasi au juhudi zinazohitajika za ujenzi wa maeneo makubwa ya kusini mwa nchi hiyo na vitongoji vya Beirut. 

Soma pia:Umoja wa Mataifa wataka dola milioni 371.4 kwa Lebanon 

"Jenerali Aoun anajulikana kama mtendaji mzuri wa maagizo," alisema mchambuzi Trombetta, akiongeza kuwa "anatarajiwa kutekeleza ajenda za waliomteua [Marekani, Saudi Arabia, na nchi nyingine zimetoa ishara kuwa ushindi wa uchaguzi wa Aoun unafungua njia kwa mipango yao ya uwekezaji, na kusimamia msaada wa kifedha ulioahidiwa kwa Lebanon kwa ajili ya ujenzi wa kimwili, ujenzi wa miundombinu, mageuzi ya kisiasa na kifedha, na kuunda upya jeshi."