Lebanon yahitaji msaada wa kimataifa kujiimarisha
24 Oktoba 2024Waziri Mkuu wa Lebanon, Najib Mikati, amesema katika mkutano wa kimataifa ulioitishwa na Ufaransa mjini Paris kwa ajili ya kuchangisha fedha za msaada, kuwa msaada wa kimataifa utaliimarisha jeshi la nchi hiyo, ambayo inashuhudia mashambulizi makubwa ya vikosi vya Israeli.
Waziri Mkuu Mikati aliongeza kwamba, serikali ya Lebanon imeazimia kuajiri wanajeshi zaidi na inaweza kupeleka wanajeshi 8,000 kama sehemu ya mpango wa kutekeleza usitishaji vita kama azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linavyoelekeza.
Soma piaUfaransa yalenga kukusanya yulo milioni 500 kwa ajili ya Lebanon:
Amesema msaada wa kimataifa unahitajika ili kufaniukisha mahitaji muhimu ya kiutu "uchokozi wa Israel haujasababisha tu mateso kwa binadamu na gharama ya maisha, lakini pia umeathiri miundombinu muhimu ya kiuchumi na kijamii."
Mikati alisema pembezoni mwa mkutano huo kuhusu Lebanon na kuongeza kwamba kuhamishwa kwa idadi kubwa ya raia kumesababisha mzozo wa kibinadamu kwa kiwango kisicho cha kawaida.
"mzozo huu unahitaji kushughulikiwa kwa dharura na jumuiya ya kimataifa."
Mikati: Azimio la UN muhimu kutekelezwa
Waziri Mkuu wa Lebanon alitoa wito wa kutekelezwa kwa azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kutumwa kwa wanajeshi 8,000 wa Lebanon kusini mwa Mto Litani, na kufufuliwa kwa juhudi za kidiplomasia ili kurejesha utulivu kusini mwa Lebanon.
Wakati wa mkutano huo, Ufaransa iliahidi kutoa dola milioni 108 kati ya dola milioni 426 zinazohitajika haraka na Umoja wa Mataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amesema mkutano wa kimataifa kuhusu hali nchini Lebanon umeweza kukusanya dola milioni 800 kwa ajili ya misaada ya kiutu na dola milioni 200 nyingine kwa ajili ya jeshi la Lebanon.
Soma pia:Watu 13 wauawa na wengine 57 wajeruhiwa huko Beirut kufuatia shambulizi la Israel
Wajumbe 70 wa serikali na mashirika 15 ya kimataifa walikutana mjini Paris wakilenga kukusanya angalau euro milioni 500 kwa ajili ya msaada wa kibinadamu na kushinikiza kusitishwa kwa mapigano.
Nako kwenye uwanja wa mapigano, Israel imeendelea kushambulia miundombinu kadhaa, na kusababisha vifo vya wanajeshi watatu wa Lebanon waliokuwa wakiokoa raia na majeruhi.
Jeshi la Israel limeomba radhi kwa mkasa huo, likisema liliwauwa kimakosa, na kuongeza kwamba linachunguza kama "liliwajeruhiwa wanajeshi kadhaa wa Lebanon kwa bahati mbaya" baada ya kulenga miundombinu ya Hezbollah.
Blinken: Watanishi wa Gaza kukutana hivi karibuni
Katika juhudi za upatanishi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken, yupo Qatar akisema wapatanishi wa Gaza watakutana hivi karibuni ili kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.
Soma pia:Blinken aanza mazungumzo huku kukiwa na mashambulizi mapya
Ziara yake inafuatia mazungumzo na viongozi wa Israel na Saudi Arabia. Qatar, Marekani, na Misri zimeongoza juhudi za upatanishi zilizofanikisha makubaliano ya kubadilishana wafungwa.
Ndani ya Gaza, Shirika la ulinzi wa raia limesema watu 770 wameuwawa kaskazini mwa eneo hilo tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi ya kuzuia kwa Hamas kujiimarisha tena.