1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lehmann amrithi Klinsmann Hertha Berlin

Josephat Charo
10 Mei 2020

Mlindalango wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani Jens Lehmenn anachukua nafasi ya Juergen Klinsmann katika bodi ya usimamizi ya Hertha Berlin, shirika la habari la Ujerumani dpa liliripoti Jumapili (10.05.2020)

https://p.dw.com/p/3c0Qv
Freundschaftsspiel Deutschland - Peru | Jens Lehmann
Picha: picture-alliance/augenklick/firo Sportphoto

Klinsmann alilazimika kujiuzulu kutoka bodi hiyo baada ya kuachia ngazi kama kocha wa mpito wa klabu hiyo ya Bundesliga mnamo mwezi Februari. Aliukosoa uongozi wa timu hiyo katika tangazo lake la kujiuzulu lakini akasema anataraji kubakia katika bodi.

Hertha hata hivyo walisema wamepoteza imani naye na hawakutaka kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani kushika wadhifa wowote katika klabu hiyo.

Lehmann, mwenye umri wa miaka 50, aliwahi kuichezea Schalke, AC Milan, Borussia Dortmund, Arsenal na VfB Stuttgart. Katika siku za hivi karibuni alikuwa kocha msaidizi wa klabu ya Augsburg inayocheza katika ligi kuu.

Kocha wa Hertha kwa sasa ni Bruno Labbadia, ambaye ataiongoza timu hiyo kwa mechi yake ya kwanza watakapokabana koo na Hoffenheim ugenini Jumamosi, huku Bundesliga ikirejea tena baada ya kusimamishwa kwa muda wa miezi miwili kutokana na janga la virusi vya corona.

(dpa)