Leipzig na Bayern ziko juu Bundesliga
24 Oktoba 2016Mabingwa mara nyingi wa Bundesliga kutoka mjini Munich , Bayern Munich, katika mchezo wa nane wa ligi ya Ujerumani wako katika nafasi waliyoizowea juu kileleni , lakini mambo hayako kawaida kwa mazowea ya ligi hiyo mara hii. Nyuma ya mabingwa hao watetezi ziko timu za RB Leipzig, Hertha Berlin, Hoffenheim na FC Kolon katika msafara wa kuifukuzilia Bayern, na katika nafasi ya sita ndipo inapatikana Borussia Dortmund makamu bingwa msimu uliopita. Vilabu vingine vyenye uwezo mkubwa kama Wolfsburg na Schalke vinatambaa bado kutoka chini ya msimamo wa ligi katika eneo la robo ya tatu ya ligi hiyo. RB Leipzig ilifanikiwa kuchupa hadi nafasi ya pili nyuma ya Bayern baada ya jana Jumapili kuicharaza Werder Bremen kwa mabao 3-1 ikiwa nyumbani.
Kocha wa RB Leipzig Ralph Hasenhüttl anasema hata hivyo haikuwa rahisi ushindi dhidi ya Werder Bremen.
"Mungu ashukuriwe tumeweza kufanikiwa, kushinda mchezo huu. Iwapo tulistahili , bila shaka , kwa jumla tulipata nafasi nyingi , kona nyingi. Lakini unaweza kuona kwamba , Bremen ni timu ambayo ina ari kubwa, timu ambayo haijifichi na ndio sababu ilikuwa vigumu, na ilibidi tutumie uwezo wetu wote kuweza kuhimili vishindo."
Inafurahisha kuona kwamba timu zilizoko juu zinatoka katika kundi la timu zinazoitwa za "kiwango cha kati", alisema hayo meneja wa spoti wa Borussia Moenchengladbach Max Eberl baada ya kipigo cha mabao 2-0 nyumbani kwa Bayern Munich siku ya Jumamosi jioni. Baada ya kung'ara katika Champions League katikati ya wiki dhidi ya Celtic Glasgow kwa kuichapa mabao 2-0 , Borussia Moenchengladbach haikuweza kufurukuta na pia nguvu ziliwaishia. Amekiri Eberl kwamba kikosi chake hakikuwa na uwezo wa kupambana katika Champions League na baada ya siku tatu kupambana katika ligi.
Inaelekea ukweli huo umedhihirika kwa Bayer Leverkusen pia ambayo ilikubali kipigo cha mabao 3 bila majibu dhidi ya Hoffenheim ambapo mshambuliaji wa Leverkusen aliyetokea Hoffenheim msimu uliopita Kevin Volland alitolewa nje kwa kadi nyekundu dakika tano tangu mchezo kuanza na kuiacha timu yake hiyo mpya ikiwa pungufu uwanjani kwa dakika takriban 85. Kevin Volland alisema.
"Nafikiri hii ilikuwa hali mbaya sana kwangu mimi. Hakuna mtu anayetamani kitu kama hicho, na pia hata timu, kupambana huku mkiwa pungufu kwa mtu mmoja . Kwa hilo hata mimi nashindwa kusema lolote, ni machungu matupu."
Hertha Berlin inashikilia nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 17 tatu nyuma ya Bayern Munich baada ya kuishinda FC Kolon kwa mabao 2-1 siku ya Jumamosi na kuizawadia Kolon kipigo chake cha kwanza msimu huu. Mlinzi wa pembeni wa Hertha Berlin aliyesababisha bao la kwanza chipukizi Mitchell Weiser anasema.
"Nafikiri baada ya mapumziko , hadi dakika ya 16 tulikuwa tumelegea kidogo na Kolon walituadhibu pia. Lakini kile ninachokiona kuwa kizuri kutoka kwetu, baada ya hapo tulifunga mlango wetu na kutoa jibu. Na huu ndio uzuri wetu na ubora wa timu yetu."
Borussia Dortmund nusura ionje kipigo siku ya Jumamosi wakati hadi kipindi cha kwanza kinamalizika wapinzani wao Ingolstadt ilikuwa ikiongoza kwa mabao 2-0. Kipindi cha pili kilishuhudia mabao manne wakati Borussia Dortmund ikijikakamua baada ya mchezo wa Chapions League dhidi ya Sporting Lisbon na kurejesha mabao matatu dakika moja kabla mchezo kumalizika na kuokoa pointi moja muhimu inayowaweka katika nafasi ya sita.
Wolfsburg ndio iliyoathirika zaidi wiki hii. Baada ya kutengana na kocha wake Dirter Hecking na kumteau kocha wa kikosi cha pili cha timu hiyo Valerien Ismail kuchukua hatamu za kukiongoza kikosi hicho hali haikuwa shwari. Kwani walibamizwa mabao 3-1 na Darmstadt. Huyu hapa kocha Valerien Ismail.
"Tulitaka kupata pointi leo. Tulitaka kujaribu , kila kitu tulichonacho. Lakini haikuwezekana. Kutokana na matokeo tumesikitishwa. Lakini nadhani, timu ilikuwa ina ari, ilijitayarisha vizuri. Ilijionesha hivyo, lakini baada ya siku tatu sidhani kama kuna mtu ambaye anaweza kuwa na matumaini makubwa. Na pia iwapo mchezaji anapewa kadi nyekundu baada ya dakika 25, ni dhahiri kwamba inakuwa vigumu sana, sana."
Hata hivyo kesho Jumanne na Jumatano viwanja kadhaa nyasi zitawaka moto wakati kutakapokuwa na kinyang'anyiro cha kombe la Ujerumani DFB Pokal duru ya pili. Mabingwa Bayern Munich watajitupa uwanjani siku ya Jumatano kupambana na majirani zao Augsburg, wakati makamu bingwa wa DFB Pokal Borussia Dortmund inapambana na Union Berlin. Siku hiyo hiyo Schalke itakuwa uwanjani kupambana na Nurmberg wakati FC Kolon inaikaribisha Hoffenheim. Kesho Jumanne Lotte inaikaribisha Bayer Leverkusen , wakati St. Pauli inakabiliana na Hertha Berlin na Borussia Moenchengladbach itapimana nguvu na VFB Stuttgart nayo Halle inaikaribisha Hamburg SV.
Premier League
Kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya Chelsea kimemletea fadhaa kocha wa Manchester United Jose Mourinho wakati akirejea katika klabu yake hiyo ya zamani ya darajani jana Jumapili.
Mourinho alionekana akiwa na uso wa huzuni jioni ya jana wakati kocha wa Chelsea Antonio Conte alionekana kufurahia sana kile alichokiona uwanjani. Mtaliani huyo aliwahamasisha mashabiki kushangiria zaidi ili kupata mabao mengine baada ya bao la nne la N'golo Kante kitu ambacho Mourinho hakufurahishwa nacho. Ripoti za vyombo vya habari vya Italia zimesema Mourinho alimwambia Conte mwishoni mwa mchezo huo, "hupaswi kushangiria kama ulivyofanya wakati ukiwa na mabao 4-0. Unaweza kufanya hivyo baada ya bao 1-0, vinginevyo inadhalilisha kwa upande wetu."
Conte alikana kufanya kosa lolote. Mourinho hata hivyo hakueleza nini alichosema katika mahojiano baada ya mchezo huo na kusema tu , maneno aliyomwambia Conte yalikuwa ni kwa yeye binafsi na sio kwa mtu mwingine.
Manchester City bado inaongoza ligi hiyo lakini kwa wingi wa mabao , ikifuatiwa na Arsenal London na Liverpool , baada ya Machester City kutoka sare ya bao 1-1 na Southamptom siku ya Jumamosi.
Hata hivyo timu hizo Manchester United na Manchester City zitarejea tena uwanjani siku ya Jumatano katika pambano la kombe la ligi duru ya nne. Kesho Jumanne Arsenal itaikaribisha Reading, Bristol itapambana na Hull City, wakati Liverpool ni wenyeji wa Tottenham Hotspurs. Chelsea itapambana na West Ham siku ya Jumatano na Southampton ina miadi na Sunderland.
Ballon d'Or
Mchezaji bora wa mwaka mara tatu duniani Cristiano Ronaldo atapambana na mchezaji mwenzake katika Real Madrid Gareth Bale kuwania tuzo hiyo ya Ballon d'Or, mpira wa dhahabu mwaka huu. Wadhamini wa tuzo hiyo , jarida la michezo la Ufaransa linatoa majina ya wachezaji 30 kwa awamu ya wachezaji watano watano leo Jumatatu.
CAF Champions League
Katika bara la Afrika , bingwa wa bara hilo kwa vilabu alipatikana jana Jumapili, ambapo Mamelodi Sundowns ya Afrika kusini ilitawazwa kwa mara ya kwanza rasmi kuwa mabingwa wa CAF Champions League licha ya kubwagwa kwa bao 1-0 na Zamalek ya Misri mjini Alexandria jana. Stanley Ohawuchi raia wa Nigeria ndie aliyeipatia Zamalek bao hilo katika dakika ya 64, lakini halikutosha kuiokoa timu hiyo wenyeji kwa kuwa Mamelodi ilikuwa tayari imepata mabao 3-0 nyumani wiki moja iliyopita katika mchezo wa kwanza uliofanyika mjini Pretoria .
Ni ushindi wa kujivunia kwasababu wababe hao wa Afrika kusini waliondolewa katika duru za mwisho za mchujo mwezi Aprili mwaka huu na kurejeshwa tena katika kinyang'anyiro hicho wakati wapinzani wao kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuondolewa. Ubingwa huo umewapa Sundowns kitita cha euro milioni 1 na lakini tatu na kupata fursa ya kuliwakilisha bara la Afrika katika michuano ya kombe la dunia la vilabu la FIFA nchini Japan mwezi Desemba.
Mbio za magari
Kwa upande wa mbio za magari , bingwa mtetezi Lewis Hamilton atawajibika kukaza uzi baada ya kurejesha uhai katika matumaini ya ubingwa wa Formula one, jana na analazimika kushinda katika mbio za Grand prix za Mexico iwapo anataka kunyakua tena ubingwa huo. Bingwa huyo alishinda mbio za Texas Grand prix nchini Marekani jana lakini Nico Rosberg anayeendesha pia gari ya Meecedes anaendelea kushikilia uongozi wa pointi 26, wakati mbio tatu zimebakia msimu huu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae / rtre
Mhariri: Iddi Ssessanga