1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leipzig yapumua nyuma ya Bayern

20 Februari 2017

RB Leipzig iliiangusha Borussia Moenchengladbach 2-1 na kupunguza pengo baina yao na vinara Bayern Munich hadi pointi tano. Bayern iliangusha pointi mbili baada ya kutoka sare ya 1-1 na Hertha Berlin

https://p.dw.com/p/2XvRS
Deutschland Borussia Mönchengladbach and RB Leipzig
Picha: picture alliance/dpa/F. Gambarini

Kocha wa Lipzig Ralph Hassenhuettl alisema timu yake ilishinda baada ya kuonyesha mchezo wa kujituma. Kilikuwa kichapo cha kwanza cha Gladbach katika ligi chini ya kocha Dieter Hecking tangu alichukua usukani mwishoni mwa mwaka jana. "Nadhani mchezo wetu kidogo ulikosa ufanisi lakini bahati mbaya tuliweza tulikabiliwa na hali kuwa walikuwa imara sana katika kipindi cha muda mfupi tu na ndicho kilitokea kwetu katika mechi chache zilizopita. Bila shaka ni kitu cha kusikitisha sana kwa sababu timu imecheza vyema sana na kwa juhudi kubwa na ingekuwa bora kama tungepata angalau pointi moja hapa". Amesema Hassenheuttl

Mjini Cologne, wenyeji walitoka sare ya 1-1 na wageni Schalke katika mechi ambayo Anthony Modeste wa Cologne alifunga bao lake la 17 msimu huu na kumfikia Pierre-Emerick Aubameyang katika orodha ya walio na waliofunga magoli mengi.

Sare hiyo imewapa Cologne pointi 33, wakati Schalke wamesonga katika nafasi ya 10 na pointi 26, juu ya Moenchengladbach kwa tofauti ya magoli.

Deutschland 1. FC Koeln v FC Schalke 04 | Tor Modeste
Anthony Modeste sasa amefunga mabao 17 sawa na Aubameyang katika Bundesliga Picha: Getty Images/Bongarts/A. Grimm

Siku ya Jumamosi, vinara Bayern Munich walihitaji bao la dakika ya mwisho kabisa kutoka kwa Robert Lewandowski na kutoka sare ya 1-1 na Hertha Berlin.

Bayern walioonekana kuwa kivuli tu cha timu iliyoibamiza Arsenal 5-1 katika Champions League, ilikuwa na nafasi chache sana za kufunga katika kipindi cha pili. Mats Hummels ni beki wa Bayern. "Berlin wamecheza kwa kujituma kuanzia dakika ya kwanza na nadhani hakuna anayeweza kulalamika kuhusu muda wa mchezo wa leo. Mapema katika kipindi cha kwanza na cha pili walipambana na wakajaribu kupunguza kasi ya mchezo. Tulijituma kwelikweli na mwishowe naamini tulistahili kupata pointi moja"

Bao la kusawazisha la Bayern lilizusha utata maana refarii aliongeza dakika tano za majeruhi, na bao la kusawazisha la Bayern likafungwa katika dakika ya sita ya muda huo kitu kilichowakasirisha sana wachezaji na kocha wa Hertha. Sebastian Langkamp ni beki wa Hertha Berlin "Kwa ujumla leo hatukuweza kupata chochote kutokana na mechi hiyo. Inasikitisha kuwa tunaondoka kwa kupata sare katika sekunde ya mwisho kabisa. Tutapaswa kuzungumzia hili maana leon tumejituma kwelikweli na kuwazuia kabisa Bayern wasishinde, lakini sasa ni kama kuna sheria iliyoandikwa kuwa hauwezi kushinda dhidi ya Bayern".

Deutschland Fußball Bundesliga Hertha BSC Berlin - FC Bayern München
Robert Lewandoswki aliondolewa aibu Bayern Munich dhidi ya HerthaPicha: Reuters/A. Schmidt

Ushindi huo umewasogeza juu na pointi 50 mbele ya Leipzig. Borussia Dortmund ilipata ushindi rahisi dhidi ya VfL Wolfsburg wa 3-0 na kusonga hadi nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi, ikiwa na pointi 37. Kocha Thomas Tuchel aliulizwa namna hali ilivyokuwa baada ya mashabiki 25,000 wa BVB kufungiwa kuhudhuria mechi hiyo. "Unaweza kuona hilo, na hata wakati kukiwa na mashabiki. Unaweza kuona wakati kumejaa na unakuwa na nafasi kubwa ya kushinda. Upande wa kusini wanakosimama mashabiki ni muhimu sana uwanjani"

Eintracht Frankfurt ilipoteza fursa yao ya kusonga hadi nafasi ya tatu, baada ya kucharazwa 2-0 na wageni Ingolsstadt. Sasa waliteremka hadi nafasi ya tano na pointi 35.

Hoffenheim ilipanda hadi nafasi ya nne baada ya kuwafunga washika mkia Darmstadt 2-0. Werder Bremena wanaokabiliwa na kitisho cha kushushwa ngazi, waliondoka katika nafasi tatu za mkia kwa kuilaza Mainz 2-0. Kwengineko, Hamburg ilitoka sare ya 2-2 na Freiburg na kuepuka eneo la kushushwa ngazi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman