1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lema arudishiwa ubunge wa Arusha

21 Desemba 2012

Mahakama Kuu ya Rufaani nchini Tanzania imetengua uamuzi wa Mahakama Kuu wa kumvua ubunge mbunge wa jimbo la Arusha kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema, na kuamua anastahiki kuwa mbunge.

https://p.dw.com/p/177Ly
Viongozi wa vyama vya upinzani vya Tanzania, Freeman Mbowe, Ibrahim Lipumba na Augustine Mrema.
Viongozi wa vyama vya upinzani vya Tanzania, Freeman Mbowe, Ibrahim Lipumba na Augustine Mrema.Picha: DW

Katika uamuzi wake Mahakama hiyo ya Rufaani imesema kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ulikuwa na kasoro kubwa hivyo kuamuru mbunge huyo kijana kurejea kwenye wadhifa wake.

Mamia ya wafuasi wa chama hicho walifurika mahakamani na baadaye waliandamana kwa shangwe na furaha kuelekea kwenye makao makuu ya chama hicho, huku wakiimba nyimbo za kusifu na kupongezana.

Akiwahutubia wafuasi wa chama chake, Mwenyekiti Freeman Mbowe alilaumu mwenendo unachukuliwa na baadhi ya watendaji katika vyombo vya maamuzi na akaitaja hukumu ya awali iliyomuengua madarakani Mbunge Lema ilikuwa ya kuegemea upande mmoja na haikuzingatia maslahi ya wananchi.

Hukumu yapokewa kwa furaha

Hukumu hiyo ya leo imepokelewa kwa hisia tofauti lakini idadi kubwa ya wale wanaofutilizia duru za kisiasa za Tanzania wanasema kuwa imekuja wakati mujarabu.

Kampeni ya pamoja ya CCM, Chadema na CUF kwa kura Zanzibar mwaka 2010.
Kampeni ya pamoja ya CCM, Chadema na CUF kwa kura Zanzibar mwaka 2010.Picha: DW

Pamoja na kupongeza hatua ya leo, CHADEMA imetangaza kile ilichokiita hakuna kulala mpaka kieleweke, ikilenga kupeleka kampeni zake za kukikabili chama tawala CCM kwenye majukwaa ya kisiasa.

Kwa hivi sasa chama hicho kinaendelea na kampeni yake iliyoipa jina la Harakati za Mabadiliko, kwa kifupu M4C, na kimesema kuwa kinatarajia kuhimiza vuguvugu la mabadiliko nchi nzima.

Kurejea bungeni kwa mbunge huyo kumeongeza nguvu ya ushawishi wa CHADEMA, ambacho kina idadi kubwa ya wabunge vijana wanaoleta upinzani mkubwa kwa hoja za serikali bungeni.

Ushindi huo wa Lema unamaliza mlolongo wa kesi nyingi zilizofunguliwa katika Mahakama Kuu baada ya uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2010.

Ripoti: George Njogopa/DW Dar es Salaam
Mhariri: Josephat Charo