1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo ni siku ya kimataifa ya Haki za Binadamu

Zainab Aziz Mhariri: Rashid Chilumba
10 Desemba 2021

Kauli mbiu ya mwaka huu katika kuiadhimisha siku ya haki za binadamu inasema binadamu wote wamezaliwa huru katika usawa, heshima na haki. Mkazo umewekwa katika juhudi za kuendeleza haki za binadamu duniani kote. 

https://p.dw.com/p/445Bl
Symbolbild I United Nations Emblem
Picha: John Angelillo/UPI/newscom/picture alliance

Azimio la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa lilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja huo mnamo mwaka 1948 kwa lengo la kusisitiza usawa wa binadamu wote bila ya kujali rangi ya mtu, dini yake, jinsia, lugha au nasaba yake ya kijamii.

Usawa wa binadamu unaenda sambamba na ajenda ya maendeleo ya mwaka 2030 ya kuhakikisha kwamba hakuna binadamu anaeachwa nyuma. Ajenda hiyo inajumuisha hatua za kutafuta masuluhisho juu ya aina za ubaguzi wenye mizizi mirefu. Na kwa mantiki hiyo umasikini, ubaguzi na tofauti za vina virefu zinahesabika kuwa ukiukaji wa haki za binadamu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Evan Schneider/UN Photo/Xinhua/picture alliance

Kuyashughulikia masuala hayo kwa ufanisi kunahitaji msimamo mpya wa kisiasa na ushiriki wa wote na hasa wale wanaoathirika. Panahitajika muundo mpya wa kijamii wa kuwawezesha wote katika kunufaika na raslimali na fursa sambamba na kuweka msingi wa kiuchumi wa kuleta haki kwa wote katika mfumo endelevu.

Umoja wa Mataifa Umesema migogoro ya fedha na majanga yaliyosababishwa na maradhi kwa muda mrefu yamewaathiri mamilioni ya vijana duniani. Bila ya haki zao kulindwa ikiwa pamoja na kuwahakikishia ajira stahiki, rika linalopitia janga la virusi vya corona litakuwamo katika hatari ya kukumbwa na madhara makubwa ya umasikini na kunyimwa usawa. Umesema dhulma iliyopo katika ugavi wa chanjo dhidi ya maradhi ni kinyume cha sheria na taratibu za kimataifa na pia ni kinyume cha moyo wa mshikamano wa kimataifa.

Watetezi wa haki za Binadamu kwenye maandamano
Watetezi wa haki za Binadamu kwenye maandamano Picha: Andreas Solaro/AFP/Getty Images

Katika kuadhimisha siku ya haki za binadamu Umoja wa Mataifa pia umesisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi za kulinda mazingira na kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Umoja wa Mataifa umesema haki za binadamu ndiyo msingi wa kung'oa mizizi ya matatizo na migogoro ya dunia kwa njia ya kuondoa tofauti miongoni mwa binadamu. Hata hivyo leo katika kuadhimisha azimio la Umoja wa Mataifa juu ya haki bado haki za binadamu zinakiukwa katika sehemu nyingi za dunia.

Chanzo: Ukurasa wa Umoja wa mataifa