1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leverkusen na Arsenal kuwania kuingia awamu ya makundi Champions League

8 Agosti 2014

Bayer Leverkusen ya Ujerumani kupambana na FC Copenhagen, na Arsenal London ina miadi na Besiktas ya Uturuki wakati timu hizo zikiwania kufuzu kuingia katika awamu ya makundi ya champions league barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/1Crbg
Fußballbundesliga - Bayer 04 Leverkusen - SV Wreder Bremen
Kikosi cha timu ya Leverkusen ya UjerumaniPicha: S.Schuermann/AFP/Getty Images

Bayer Leverkusen ya Ujerumani iliyoshika nafasi ya nne katika ligi ya Ujerumani Bundesliga msimu uliopita itakuwa ugenini kupambana na FC Copenhagen katika kinyang'anyiro cha kuwania kufuzu kuingia katika duru ya makundi ya Champions League barani Ulaya kufuatia upangaji wa duru ya awali ya mtoano katika kinyang'anyiro hicho.

Napoli ya Italia itaoneshana kazi na Athletic Bilbao ya Uhispania na Arsenal London inakumbana na Besiktas ya Uturuki. Mabingwa wa zamani mara mbili Porto pia wanajikuta katika pambano gumu ambapo wamepangwa dhidi ya Lille ya Ufaransa, wakati klabu hiyo kutoka Ufaransa itakuwa nyumbani katika mchezo wa kwanza.

Europa League Hamburg gegen Celtic
Celtic Glasgow wamepata nafasi ya pili kushiriki Champions League UlayaPicha: AP

Celtic yapata nafasi nyingine

Mabingwa wa Scottland Celtic Glasgow , ambayo imerejeshwa katika kinyang'anyiro hicho baada ya wapinzani wao katika awamu ya tatu ya michuano ya mtoano katika champions league msimu huu Legia Warsaw kuondolewa kwa kumchezesha mchezaji ambaye hakustahili kucheza katika ushindi wao wa mabao 3-0 dhidi ya Celtic na kufikisha ushindi wa jumla wa mabao 6-1 , watakutana na mabingwa wa Slovenia Maribor katika awamu hii.

Mabingwa wa zamani wa Champions League Steaua Bucharest wamepangwa kuumana na Ludogorets Razgrad ya Bulgaria. Michezo ya kwanza itafanyika Agosti 19 na 20 na mchezo wa marudio utakuwa Agosti 26 na 27.

Ligi ya Uingereza , Premier league inaanza rasmi jumamosi wiki ijayo , wakati timu zile kubwa zinaonekana kujiimarisha kwa wachezaji wapya pamoja na makocha kuweza kuhimili vishindo vya ligi hiyo ngumu duniani.

Kocha mpya wa Manchester United Louis van Gaal amekwisha onesha uwezo wake katika klabu hiyo ambayo inataka kurejea haraka katika nafasi za juu katika ligi hiyo ya Uingereza baada ya msimu ambao umewasononesha sana mashabiki wa klabu hiyo ambao wamezowea mafanikio.

Baada ya msimu usiokuwa mzuri chini ya kocha wa zamani David Moyes , Man United ilichukua hatua za haraka kumteua kocha mzoefu Mholanzi Louis van Gaal kurejesha heshima ya klabu hiyo maarufu duniani.

Van Gaal na Man U

Licha ya kuwa alikosoa sana ziara ndefu ya Marekani , Van Gaal ameiongoza Manchester United kupata ushindi mara tano dhidi ya wapinzani watano ambao ni timu kongwe kama Real Madrid, AS Roma , Inter Milan na Liverpool.

Arsenal London pia imo mbioni kuonesha kuwa msimu huu sio kama uliopita , baada ya kupata huduma ya mshambuliaji kutoka Barcelona Alexis Sanchez, Mathieu Debuchy na Calum Chambers pamoja na mlinda mlango David Ospina.

Chelsea London haikuachwa nyuma , ambapo imepata saini ya mshambuliaji hatari Diego Costa na mchezaji wa kati wa Barcelona Cesc Fabregas.

Mlinda mlango kutoka Uhispania Pepe Reina amejiunga na mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich jana Ijumaa na atakuwa na mabingwa hao akiwa mchezaji namba mbili baada ya Manuel Neuer. Reina mwenye umri wa miaka 31, alifanyiwa uchunguzi wa kiafya siku ya Alhamis.

Torwart Pepe Reina
Pepe Reina mlinda mlango mpya wa Bayern MunichPicha: Getty Images

"Nimekuja hapa kwasababu nataka kushinda mataji mengi iwezekanavyo," amesema Reina katika tovuti ya timu hiyo ya mjini Munich. Reina alikuwa ameazimwa msimu uliopita na Napoli ya Italia kutoka Liverpool ya Uingereza na kabla ya hapo aliichezea Barcelona na Villarreal za Uhispania.

Suarez aomba kupunguziwa adhabu

Mahakama ya upatanishi katika soka CAS imeanza kusikiliza rufaa ya mshambuliaji wa Uruguay Luis Suarez kuhusiana na hatua ya kupigwa marufuku kuhusika na masuala ya mchezo wa kandanda baada ya kumtafuna begani mlinzi wa Italia Giorgio Chiellini katika mchezo wa kombe la dunia.

Chama cha umoja wa wachezaji wa kandanda FIFPro kimetoa wito wa kupunguzwa kwa adhabu dhidi ya Suarez jana Ijumaa. Mahakama hiyo ya upatanishi imesema hata hivyo kuwa uamuzi utatolewa siku chache baada ya kukamilika kwa hatua za kusikiliza kesi hiyo .

Fußball FIFA World Cup 2014 Luis Suarez Liverpool
Mshambuliaji wa Barcelona Louis SuarezPicha: picture-alliance/dpa

Kesi hiyo inafanyika kwa faragha . Suarez ambaye amejiunga na Barcelona kutoka Liverpool ya Uingereza ameshindwa katika rufaa ya kwanza iliyosikilizwa na kamati ya nidhamu ya shirikisho la kandanda duniani FIFA.

Wachezaji watano wa zamani pamoja na wengine watano ambao ni watuhumiwa walitarajiwa kufika mbele ya mahakama ya uhalifu jana mwanzoni mwa kesi itakayochukua siku kumi kwa madai ya kuhusika kwao katika kashfa ya upangaji wa matokeo ya michuano ambayo imelitikisa soka la Australia mwaka jana.

Watuhumiwa hao 10 , ikiwa ni pamoja na Sanel Kuljic ambaye amestaafu soka la kimataifa wameshtakiwa kwa kuingilia kwa nia ya kufanya udanganyifu wa matokeo katika michezo 18 ya ligi ya nchi hiyo.

Wachezaji hao wanadaiwa kuwa wamepokea kati ya euro 7,000 hadi 25,000 kwa kila mchezo ambapo wametakiwa kuingiza ushawishi wao na kubadilisha matokeo , na kuwafanya wasaidizi wao kutoka Austria , Albania, Serbia na Chechnya kupata faida katika kamari.

Drogba atundika madaluga timu ya taifa

Na katika bara la Afrika mshambuliaji mkongwe wa timu ya taifa ya Cote D'Ivoire Didier Drogba ametangaza kujiuzulu rasmi katika timu hiyo ya taifa jana Ijumaa baada ya kupachika wavuni mabao 61 katika michezo 103 aliyoitumikia timu hiyo ya Tembo la Cote D'ivoire.

WM 2014 Gruppe D 1. Spieltag Elfenbeinküste Japan
Didier Drogba wa Cote D'IvoirePicha: Reuters

Wakati huo huo Emad Mateb yuko tayari kuisaidia Al-Ahly ya Misri ambayo inamatatizo ya kupachika mabao wavuni kufika katika nusu fainali ya michuano ya kombe la shirikisho la kandanda barani Afrika CAF mwishoni mwa juma hili.

Mashetani wekundu hao wa mjini Cairo wako nyumbani kwa Nkana Red Devils wa Zambia na sare tu itaiwezesha timu hiyo ya mjini Cairo kufikia katika hatua hiyo ya timu nne za mwisho katika kinyang'anyiro hicho.

Michezo mingine ni kati ya Coton Sport ya Cameroon ikipambana na AC Leopards ya Congo Brazzaville , na ASEC Mimosas ya Cote D'Ivoire inachuana na Real Bamako ya Mali.

Katika kundi B pia kutakuwa na mchezo kati ya Etoile Saleh ya Tunisia ikipambana na Sewe San Pedro Cote D'Ivoire. Mshindi wa kila kundi na timu inayofuatia zitaingia katika nusu fainali.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / ape / rtre / dpae

Mhariri : Yusuf , Saumu