Lewandowski anaondoka au haondoki?
26 Aprili 2013Taarifa fupi ya mabingwa hao a Bundesliga imekanusha madai hayo . Bayern ambao waliwashinda Barcelona mabao manne kwa sifuri katika mchuwano wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa hajawasema kama wanafanya mazungumzo na wawakilishi wa mchezaji huyo raia wa Poland. Bayern imeshangaza mashabiki wa Dortmund siku moja kabla ya timu yao kuwachabanga Real Madrid magaoli manne kwa moja katika Ligi ya Mabingwa kwa kutangaza kuwa wamefikia mkataba na Dortmund wa kumsajili kiungo wake mshambulizi Mario Goetze kwa kiasi kinachoripotiwa kuwa euro milioni 37.
Mfungaji bora wa Bundesliga Lewandowski ambaye alifunga mabao yote manne ya Dortmund dhidi ya Real, amekataa kusaini mkataba mpya kuendelea mwaka wa 2014 na huenda akaondoka mwishoni mwa msimu huu. Lakini yeye, tofauti na Goetze, hana kipengele cha kuuvunja mkataba wake na huenda akalazimika kusalia katika klabu hiyo. Wawakilishi wa mchezaji huyo wamesema Alhamisi wiki hii kuwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24 hatabakia katika klabu hiyo, lakini kufikia sasa hajazungumzia hali hiyo. Kiwango cha ushindi uliosajiliwa na timu za Bayern Munich na Borussia Dortmund katika mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Champions League, dhidi ya timu mahiri za Uhispania Barcelona na Real Madrid, kinathibitisha kuimarika kiwango cha soka la Ujerumani, Bundesliga. Ushindi wa Bayern wa magoli manne kwa sifuri dhidi ya Barca, nao Dortmund kuwanyamazisha Real Madrid manne kwa moja, ulifanya gazeti maarufu la kichezo Ujerumani kuandika ripoti yenye kichwa: Ujerumani 8, Uhispania 1: Bayern na Dortmund wameiteka Ulaya!
Wakati Uhispania ikiendelea na Uchunguzi wa ni kwanini Barca na Real zilifanya vibaya sana dhidi ya wapinzani wa Bundesliga, Ujerumani inaota kuhusu „Der Klassiker“ kama Bayern watapambana na Dortmund katika fainali itakayoandaliwa katika uwanja wa Wembley jijini London mnamo Mei 25.
Bayern Munich Rais wa Shirikisho la Soka Ujerumani – DFB Wolfgang Niersbach amesema Bayern na Dortmund zimedhihirisha kiwango cha juu cha soka ya Ujerumani. Kwamba hiyo inahusisha Bundesliga, vilabu binafsi na timu ya taifa. Anaongeza kuwa sasa wanaweza kuota kuhusu fainali ya timu mbili zote za Ujerumani.
Naye kocha wa timu ya taifa ya soka ya Ujerumani „Die Manshaft“ Joachim Löw amesema huku wachezaji wake 14 wakiwa bado katika kinyang'anyiro hicho, pamoja na Mesut Ozil na Sami Khedira wote wa Real Madrid, ujuzi huo unaweza kukisaidia kikosi cha taifa kabla ya dumba la kombe la dunia mwaka ujao nchini Brazil. Gazeti la Bild ia limepima mafanikio ya timu za Ujerumani ikilinganishwa na kuporomoka timu nne za Premier League ya England, Manchester United, Chelsea, Manchester City na Arsenal, kushindwa kufuzu katika nusu fainali.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef