Lewandowski apigwa na kiripuzi
12 Novemba 2016Mshambuliaji wa Poland Robert Lewandowski aliangukiwa na fashifashi iliyorushwa kutoka jukwaa la watazamaji katika pambano lililokuwa na hamasa nyingi jana Ijumaa , lakini hatimaye ndie aliyetoka uwanjani akitabasamu , baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Romania.
Mashabiki wa Romania walirusha fashifashi dhidi ya nyota huyo wa Bayern Munich katika dakika ya 53. Alihitaji matibabu kidogo wakati refa Damir Skomina aliwakusanya wachezaji wa pande zote katikati ya uwanja.
Baada ya mchezo huo kusitishwa kwa muda , Lewandowski aliweza kufunga mabao mawili baada ya dakika 84 pamoja na penalti ya dakika za mwisho.
Kwa upande wa watazamaji , mashabiki kutoka kila upande walirushiana fashifashi. Baadhi zilizorushwa na mashabiki wa nyumbani ziliangukia uwanjani , na kusababisha kucheleweshwa mchezo huo kuanza kabla ya mapumziko. Mashabiki 12 wa poland walikamatwa kabla ya mchezo huo baada ya kuigana katika baa katikati ya mji na mapambano na polisi nje ya uwanja.
Nahodha wa Mexico Rafael Marquez alifunga bao ushindi katika dakika ya 89 wakati Mexico ilipoishangaza Marekani kwa ushindi wa mabao 2-1 katika pambano la kusisimua la kufuzu kucheza katika fainali za kombe la dunia kati ya timu hizo mbili mahasimu wakubwa jana Ijumaa.
Marquez , mwenye umri wa miaka 37, alifunga kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Miguel Layun katika dakika za mwisho na ambapo Bobby Wood alisawazisha hapo kabla bao la Mexico lililofungwa na Layun katika dakika ya 20 ya mchezo.
Matokeo mengine katika michezo ya kanda ya shirikisho la CONCACAF ni Honduras ilikandikwa bao 1-0 na Panama , Trinidad na Tobago ilisalimu amri mbele ya Costa Rica kwa kufungwa mabao 2-0.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Sylvia Mwehozi